Kesi kupinga zuio la Bunge ‘live’ yafikia patamu

28Jun 2016
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kesi kupinga zuio la Bunge ‘live’ yafikia patamu

MAHAKAMA Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, inatarajia kupokea majibu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na watu 11 wakipinga kuzuiliwa matangazo ya moja kwa moja (live)ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, Julai 11, mwaka huu.

Kesi hiyo imefunguliwa mahakamani hapo dhidi ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na AG, ilitajwa tena jana mbele ya Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambari.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abubakar Mrisho, aliomba kuwasilisha majibu ya kesi hiyo dhidi ya Waziri na AG, Julai 11, mwaka huu.

Nao upande wa walalamikaji uliongozwa na Mawakili, Peter Kibatala na Omary Msemo, ulidai kuwa, kama kutakuwa na haja ya kujibu hoja zitakazowasilishwa na Jamhuri watafanya hivyo Julai 15, mwaka huu.

Jaji Kiongozi Wambari alisema kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu, Ama-Isario Munisi na Said Kihiyo, ambao kwa sasa wanaendelea na vikao vya kesi za mauaji.

Aliutaja upande wa walalamikiwa uwasilishe majibu yao Julai 11, mwaka huu na walalamikaji endapo watakuwa na majibu ya hoja hizo wawasilishe Julai 15, mwaka huu.

Katika madai ya msingi, walalamikaji wanaiomba mahakama itangaze kuwa raia wana haki kikatiba ya kupata majadiliano ya Bunge chini ya Ibara ya 18 (b) na (d) na Ibara ya 29(1) ya Katiba.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa