Kesi mbunge, 'house boy' yaanza kunguruma kortini

26May 2020
Allan lsack
Arusha
Nipashe
Kesi mbunge, 'house boy' yaanza kunguruma kortini

KESI ya wizi iliyofunguliwa na Mbunge wa zamani wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Anjellah Kizigha, dhidi ya mfanyakazi wake wa ndani, William Mlewa, akimtuhumu kumwibia Sh. milioni saba, imeanza kusikilizwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Maromboso jijini Arusha.

Mashahidi watatu kati ya wanne wa upande wa mashitaka katika kesi hiyo, wamedai mahakamani kuwa hawakumwona mtuhumiwa William Mlewa akiiba kiasi hicho cha fedha nyumbani kwa mlalamikaji.

Katika kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Neema Mchomvu, mashahidi hao kwa nyakati tofauti walidai mahakamani huko, kuwa hawakumwona mshitakiwa ambaye ni kijana wa kazi nyumbani kwa mlalamikaji akiiba fedha hizo, zaidi ya kumsikia akimwomba msamaha mlalamikaji kwamba alichukua fedha hizo.

Mbele ya Hakimu Mchomvu, mlalamikaji alidai kuwa kwa mara ya kwanza Februari, mwaka huu, kulitokea wizi wa fedha nyumbani kwake na walikuwa wakiishi watu watatu akiwamo mlalamikaji, Frank Gerald na William Mlewa.

"Mara ya kwanza zilipotea fedha Sh. milioni 1.7 na baadaye zikapotea Sh. milioni mbili na mara ya mwisho wiki mbili zilizopita, zilipotea fedha zilizokuwa kwenye mfuko niliokuwa nimeuhifadhi stoo na ndani, hakuna mtu aliyejua nilipohifadhi fedha tofauti na William, lakini nilipomuuliza alikataa," alidai.

Aliendelea kudai kuwa baadaye alikwenda kuangalia tena stoo na kuukuta mfuko wa fedha na alipoufungua, ndipo alipogundua kuwa kuna kiasi cha fedha hizo zimechomolewa.

"Niliamua kuchukua kiasi kilichobaki na kuweka katika bahasha tatu na nilikwenda kanisani kutoa sadaka na baadaye nilitoa taarifa polisi," alidai.

Shahidi wa kwanza katika shauri hilo, Daniel Siuchi, alidai mahakamani kuwa alikwenda nyumbani kwa Kizigha kufanya kazi na ndani ya nyumba hiyo, alimsikia mtuhumiwa akimwomba msamaha mlalamikaji kwamba alizichukua Sh. milioni tatu na kuzitumia kwa mambo yake.

Hata hivyo, shahidi huyo alipoulizwa na hakimu kama alimwona mtuhumiwa akiiba fedha hizo, shahidi huyo alidai hakumwona.

Akihojiwa na wazee wa baraza hilo, shahidi mwingine, Tizo Yahaya (25), ambaye ni mtunza bustani, pia alidai hakumwona mtuhumiwa akiiba fedha hizo, lakini alimsikia mlalamikaji akidai kwamba fedha zake zimekuwa zikipotea mara kwa mara katika miezi Machi na Aprili mwaka huu.

Shahidi mwingine, Frank Gerald (45), ambaye alikwenda kuchomelea vyuma nyumbani kwa mlalamikaji, alidai mahakama huko kuwa mlalamikaji aliwanyima chakula kwa muda wa wiki nzima ili waseme ni nani aliyeiba fedha hizo.

Gerald pia alidai kuwa hakumwona mtu yeyote akiiba fedha hizo na kwamba mlalamikaji alifikia hatua ya kuvua nguo zake ili kuwalaani watu wote walioiba fedha hizo, huku akichukua fedha zilizopatikana kwenye begi la mtuhumiwa na kuziweka kwenye bahasha tatu na kuahidi kuzipeleka kanisani kama sadaka, ili Mungu amwonyeshe aliyeiba fedha zake.

"Mama alipotoka kanisani alirejea nyumbani na kutuuliza kwa mara nyingine ni nani ameiba fedha zake, lakini tulikana wote, ghafla William alimfuata chumbani akamwambia 'Mama ninaomba unisamehe, mimi ndiye niliyechukua fedha'," alidai.

Katika kesi hiyo, Hakimu Mchomvu aliwazuia mlalamikaji na shahidi wake,Tizo Yahya, kuzungumzia tukio la kuungua kwa uji kwa mtuhumiwa katika maelezo yao na kuwataka wajikite katika kesi ya msingi ya wizi wa fedha hizo.

Baada ya kumaliza kutolewa ushahidi huo, Hakimu Mchomvu alihahirisha kesi hiyo hadi Juni 5 mwaka huu, itakapoendelea kusikiliza ushahidi wa mwisho upande wa mashitaka.

Habari Kubwa