Kesi vigogo Acacia yapigwa kalenda

08Dec 2018
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kesi vigogo Acacia yapigwa kalenda

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu,  Dar es Salaam, imepiga kalenda  kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa Migodi ya Pangea, North Mara Exploration na Bulyanhulu, Deogratius Mwanyika na wenzake mpaka Desemba 21, mwaka huu itakapotajwa.

Jana kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Huruma Shaidi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi,  Mutalemwa Kishenyi, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika aliomba tarehe ya kutajwa.

Wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa, alidai kuwa mara ya mwisho kesi hiyo ilipotajwa, Jamhuri ilidai kwamba bado  kuna baadhi ya vielelezo wanavifanyia kazi lakini 
Kishenyi alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo ni mpana kwamba kuna nyaraka zinafanyiwa kazi.

Hakim alisema kesi hiyo itatajwa Desemba 21, mwaka huu na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.

Mbali na Mwanyika washtakiwa wengine ni Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Bulyanhulu Alex Lugendo,  Mkurugenzi Mtendaji wa Pongea, North Mara na Bulyanhuku Assa Mwaipopo, kampuni ya Mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza  Oktoba 17,mwaka huu.

 Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 39, yakiwamo ya utakatishaji na kukwepa kodi zaidi ya USD  112 milioni.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama , mashtaka saba ya kughushi , mashtaka 17 ya utakatishaji wa fedha, Kuwasilisha nyaraka  za uongo  kwa  Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), shtaka moja, kuongoza uhalifu wa kupangwa, mashtaka nane ya kukwepa kodi na shtaka moja la kutoa Rushwa.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Aprili 11, 2008 na Juni 30,2007 katika sehemu tofauti za jiji la Dar es Salaam, Kahama Mkoani Shinyanga, Tarime Mara, Biharamulo Kagera maeneo ambayo yapo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 Maeneo mengine ambayo washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo ni katika mji wa Johannesburg, Afrika Kusini, Toronto Canada na nchini  Uingereza.

Aidha mshtakiwa Mwanyika  na Lugendo, wanadaiwa kutoa msaada katika kusimamia mkakati wa kihalifu kwa nia ya kupata faida.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutoa tamko la uongo kwa kamishna Generali wa TRA huko Biharamulo kwa nia ya kukwepa kulipa kodi ya Dola 9,309,600 ambayo ilipaswa kulipwa kwa TRA.

Washtakiwa Mwanyika na Lugendo wanadaiwa kuwa kati ya Desemba 2009 na Desemba 31 2018 katika maeneo tofauti ndani na nje ya nchi ya Tanzania kwa pamoja na wengine ambao hawapo mahakamani, walisaidia mgodi wa North Mara kuhamisha fedha kiasi cha USD 374,243,943,45 huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa ya kughushi na kukwepa kodi.

Pia washtakiwa wanadaiwa kati ya Novemba 2,  2012 na Novemba 27, 2015 huko Shinyanga walitoa Rushwa ya Sh. 718,520,001.76 kwa Hussein Kashindye ambaye  ni mkuu wa upelelezi makosa ya jinai wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kumshawishi ili aweze kuachana na uchunguzi wa makosa ya jinai yaliyokuwa yametendwa na Mgodi wa Bulyanhulu.

Katika shtaka la kughushi washtakiwa hao wakiwa na nia ya ulaghai waligushi mkataba wa mkopo wakitaka kuonyesha kwamba Aprili 30, 2014 Kampuni ya Pangea limited ilikubali kukopa USD 90,000,000 ikiwa na riba kutoka benki ya kimataifa ya barrick huku wakijua kuwa siyo kweli.

Katika shtaka la kutoa nyaraka ya uongo, mshtakiwa Mwanyika anadaiwa Aprili 30, 2018 huko BOT iliyopo wilaya ya ilala, kwa makusudi aliwasilisha  nyaraka ya uongo ya mkopo baina ya kampuni mgodi wa Bulyanhulu na Barrick international bank Corp kwa madhumuni ya kuonesha kuwa, kati ya June 2001 na Desemba 13, 2007 Bulyanhulu walijipatia mkopo usio na faida wa USD 416,100,000 kutoka Barrick.

Habari Kubwa