Kesi ya kujiuzulu Ndugai kuanza leo

26Jan 2022
Kulwa Mzee
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kesi ya kujiuzulu Ndugai kuanza leo

JOPO la majaji watatu leo linatarajia kuanza kusikiliza kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia kupinga kujiuzulu kwa aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai na hatua za kupata spika mwingine kwa madai utaratibu ni batili.

aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Jopo la majaji watatu linaloongozwa na Mwenyekiti Jaji John Mugeta, linatarajia kusikiliza shauri hilo namba mbili la mwaka 2022 lililofunguliwa chini ya hati ya dharura.

Wengine kwenye jopo hilo ni Benhaji Masoud na mwingine ambaye atatajwa baadaye.

Mleta maombi katika kesi hiyo ni Mbatia, wakati mjibu maombi wa kwanza ni Ndugai, wa pili ni Katibu wa Bunge na mdaiwa wa tatu ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Mjibu maombi wa pili na watatu wanawakilishwa na Mawakili Wakuu wa Serikali, Mussa Mbura, Deodatus Nyoni, Andrew Chang'a na Wakili wa Serikali Stanley Kalokola.

Mjibu maombi wa kwanza na wakili wake wanatarajiwa kufika mahakamani kusikiliza shauri hilo ambalo lilikwama kuendelea juzi.

 

Mahakama ilikataa kutoa siku 14 kwa mawakili wa serikali waliokuwa wameziomba kwa ajili ya kujibu kiapo kinzani badala yake walitakiwa hadi jana saa 8.30 mchana wawe wamewasilisha majibu hayo.

Wakili wa mleta maombi, Mpare Mpoki, alidai dharura katika shauri hilo ipo kwa sababu kuna uchaguzi wa spika.

"Tunachoharakia uchaguzi wa spika usifanyike, busara ya mahakama hii inatakiwa itoke kabla ya uchaguzi wa spika Januari 31, mwaka huu.

" Mahakama pekee ndiyo inayoweza kusimamisha uchaguzi wa spika," alidai Mpoki.

Juzi mahakama iliagiza mjibu maombi wa kwanza Ndugai apelekewe hati ya wito mkononi badala ya email kama ilivyofanyika, kabla ya jana saa 8.30.

Mbatia anapinga utaratibu uliotumiwa na aliyekuwa Spika wa Bunge Job Ndugai kujiuzulu na mchakato wa kupata spika mwingine.

"Katiba imeweka utaratibu, spika akitaka kujiuzulu anatakiwa kwenda kufanya hivyo kwa watu waliomchagua ambao ni wabunge.

"Utaratibu uliotumiwa na Ndugai ni batili haukubaliki kikatiba," alidai Mbatia.

Ndugai alijiuzulu uspika Januari 6 mwaka huu na Januari 21 mwaka huu, Dk. Tulia Ackson aliteuliwa kugombea uspika.

Habari Kubwa