Kesi ya Mbowe: Marufuku majina ya JPM, Samia kutajwa

20Jan 2022
Kulwa Mzee
Dar es Salaam
Nipashe
Kesi ya Mbowe: Marufuku majina ya JPM, Samia kutajwa

JAJI Joackim Tiganga anayesikiliza kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu amesitisha maswali ya wakili wa utetezi yanayomtaja Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli na Rais Samia Suluhu katika kesi hiyo wakati hawapo kortini.

Maswali hayo ya kutaja Rais wa awamu ya tano na sita yaliibuliwa jana na wakili wa utetezi, Faraja Mangula, wakati akimuhoji shahidi wa 10 wa Jamhuri, Inspekta Innocent Ndowo, kutokana na ushahidi wake.

Wakili Mangula alihoji swali akitaka shahidi aeleze cheo cha Inspekta alikipata wakati wa Rais wa awamu ya tano au ya sita.

Akijibu shahidi alidai haelewi swali lake ndipo Jaji Tiganga alipomuhoji wakili huyo kuwa swali la nani alikuwa Rais anataka kujenga kitu gani.

Wakili Mangula alidai anataka kujenga msingi, lakini Jaji alihoji huo msingi ndio atengeneze kupitia Rais aliyekuwapo madarakani.

"Nilishatoa maelekezo ya kutaja majina ya watu ambao hawapo mahakamani, lakini nataka kujiuliza kuhusu kuuliza maswali ya Rais wa awamu ya tano au la unachotaka hapo ni nini? Alihoji Jaji Tiganga.

Wakili Mangula alidai katika kesi hiyo kuna watuhumiwa walikamatwa awamu ya tano na wengine awamu ya sita, lakini aliomba kuuliza maswali kwa namna nyingine.

Shahidi alidai alipewa vielelezo zikiwamo simu kufanya uchunguzi na hajui kama kuna ugaidi au hakuna.

Inspekta Ndowo alidai katika simu kulikuwa na mazungumzo ya watuhumiwa na mazungumzo ya muda mrefu yalikuwa dakika tisa na alipohojiwa sauti zao ziko wapi aliomba asijibu swali hilo kwa sababu za kiusalama.

Shahidi anadai wakati wanafanya uchunguzi hawakuwa na maslahi na kesi hiyo, hivyo si sahihi kwamba waliamua kuficha baadhi ya taarifa katika kesi hiyo.

Akihojiwa na Wakili Fredrick Kihwelo kuhusu kampuni ya Celebrite anayodai inatengeneza software kwamba ni kampuni ya kijasusi ya kidigitali ya nchi ya Israeli alidai hafahamu.

Alidai hafahamu kama kampuni hiyo pia inahusishwa na unyanyasaji wa waandishi wa habari na wanaharakati duniani.

Akihojiwa na Wakili John Mallya alidai kielelezo C ni simu ya mshtakiwa Halfani Bwire ambayo katika uchunguzi hakukuta kitu cha kuchukua.
Anadai ujumbe wenye matokeo hasi alioukuta hakuwa na sababu ya kuuweka.

Anadai alifanya uchunguzi Julai 2021, ushahidi amekuja kutoa Januari 2022 ni takribani miezi mitano.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mbowe, Halfani Bwire, Adamu Kasekwa na Mohammed Ling'wenya ambao wanakabiliwa na mashtaka sita ikiwamo kula njama kufanya vitendo vya kigaidi kati ya Mei mosi na Agosti 5, mwaka 2020.

Habari Kubwa