Kesi ya Membe dhidi ya Musiba  Agosti 6

03Jul 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kesi ya Membe dhidi ya Musiba  Agosti 6

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imekubali ombi la kuongezewa muda walalamikiwa Cyprian Musiba, Mhariri wa gazeti la Tanzanite na Mchapishaji wake kuwasilisha majibu katika kesi ya madai ya fidia ya Sh.bilioni 10 iliyofunguliwa ba  Waziri  wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernad Membe.

Kadhalika, mahakama hiyo imetoa siku saba kwa walalamikiwa kuwasilisha majibu ya maombi hayo ndani ya siku saba na kwamba mlalamikaji kama atakuwa na cha kujibu afanye hivyo kabla ya Agosti 6, mwaka huu kesi ya msingi itakaposikilizwa.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Joaquine Demelo, baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili kuhusu walalamikiwa kuongezewa muda wa kuwasilisha majibu ya maombi ya Membe badala ya upande mmoja.

Jaji alisema mahakama yake imekubali maombi ya walalamikiwa kuwasilisha majibu nje ya muda na kesi ya msingi itasikilizwa Agosti 6, mwaka huu.

"Lazima pande zote zisikilizwe ijulikane haki ni ya nani, tutasikiliza kesi ya msingi Agosti 6, mwaka huu, walalamikiwa wawasilishe majibu ya maombi ya msingi ndani ya siku saba," alisema Jaji Demelo.

Katika kesi ya msingi, Musiba anadaiwa kumtuhumu  na kumkashifu Membe kuwa anamhujumu Rais Dk. John Magufuli na kwamba mbinu mojawapo ya kukamilisha hujuma hizo ni maandalizi ya kampeni za kugombea urais 2020.

Habari Kubwa