Kesi ya Sabaya kuendelea leo

13Oct 2021
Allan Isack
ARUSHA
Nipashe
Kesi ya Sabaya kuendelea leo

KESI ya uhujumu uchumi namba 27 inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, inatarajiwa kuendelea kunguruma leo Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa shahidi wa nne kupanda kizimbani kutoa ushahidi.

Mbali na Ole Sabaya washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Silvester Nyengu (26), Enock Togolani (41), Watson Mwahomange (27), John Odemba, Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31), wanaokabiliwa na mashtaka matano.

Hadi sasa mashahidi watatu wa Jamhuri katika shauri hilo la uhujumu uchumi wameshapanda kizimbani kutoa ushahidi wao mahakamani huko.

Katika kesi hiyo, shtaka la kwanza ni la kuongoza genge la uhalifu kinyume cha Sheria ya Uhujumu Uchumi kifungu cha 57(1) na 60(2) na linawakabili washtakiwa wote.

Ilidaiwa mahakamani huko kwamba kwa pamoja washtakiwa hao, Januari 22 mwaka huu, katika maeneo tofauti ya Jiji la Arusha, walifanya vitendo vya uhalifu kwa kujipatia fedha kiasi cha Sh. milioni 90 kwa manufaa yao.

Shtaka la pili la kujihusisha na vitendo vya rushwa linamkabili mshtakiwa wa kwanza peke yake, akituhumiwa kwenda kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kifungu cha 15(1B,2) sura ya 329 na marejeo yake ya mwaka 2019.

Ilidaiwa mahakamani huko, kwamba Januari 22 mwaka huu, eneo la kwa Murombo jijini Arusha, Sabaya alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kumtaka Francis Mroso kumpatia fedha kiasi cha Sh. milioni 90 kwa kumshinikiza ili asitoe taarifa za jinai  za mtu huyo za madai ya ukwepaji kodi.

Shtaka la tatu ni la kujihusisha na vitendo vya rushwa, linamkabili mshakiwa wa kwanza peke yake. Ilidai kwamba Januari 22, mwaka huu, Sabaya akiwa katika eneo la Kwa Morombo jijini Arusha, alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kujipatia fedha kiasi cha Sh. milioni 90 kutoka kwa Francis Mroso ili asitoe taarifa za jinai  za mtu huyo za madai ya ukwepaji kodi.

Shtaka la nne ni la matumizi mabaya ya madaraka, linamkabili Sabaya peke yake. Ilidaiwa mahakamani huko kwamba Januari 22, mwaka huu, Ole Sabaya, akiwa katika eneo la Kwa Murombo jijini Arusha, alitumia vibaya nafasi yake ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, alimtisha Francis Mroso kumfungulia mashtaka ya kukwepa kodi na kitendo hicho ni kinyume cha kifungu cha 15(9) cha Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Shtaka la tano ni la utakatishaji wa fedha na linawakabili washtakiwa wote saba. Inadaiwa kuwa Februari 22, mwaka huu, Ole Sabaya kwa kushirikiana na wenzake, wakiwa katika eneo la Kwa Murombo jijini Arusha, walijipatia fedha kiasi cha Sh. milioni 90, wakitambua kwamba kufanya hivyo ilikuwa ni zao la vitendo vya rushwa.

Habari Kubwa