KESI YA ZITTO: Shahidi adai kupokea majeruhi watatu

17Jul 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
KESI YA ZITTO: Shahidi adai kupokea majeruhi watatu

DAKTARI Ernest Kiluhungwa (46), kutoka Kituo cha Afya Nguruka katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Mkoa wa Kigoma, amedai mahakamani kwamba aliwapokea na kuwapa matibabu majeruhi watatu baada ya kudaiwa kupigwa risasi na askari polisi eneo la Mwanduhubandu.

Kadhalika amedai kuwa baada ya kuwapa matibabu walilazwa katika kituo hicho, lakini alipigiwa simu na askari polisi kwamba wamewachukua majeruhi hao kwa kuwa ni wahalifu na wako salama.

Dk. Kiluhungwa alitoa ushahidi huo jana dhidi ya kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, inayosikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka akisaidiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Nassoro Katuga na Wankyo Simon.

Alidai kuwa alihamishiwa katika kituo hicho mwaka 2017 na kwamba wapo madaktari watatu na wauguzi.

Akiongozwa na Wakili Katuga, shahidi alidai kuwa Oktoba 18, 2018 alikuwa Kituo cha Afya cha Nguruka tangu asubuhi na kwamba alikuwa daktari wa zamu wengine walikuwa na shughuli nyingine nje ya kituo.

"Ilipofika saa 12 jioni nilipokea majeruhi watatu wakiwa mahututi waliosindikizwa na watu wengine wawili, niliwakagua mmoja alikuwa amepigwa risasi sehemu mbili tofauti tumboni, wawili walijeruhiwa kifuani na mabegani walikuwa wakitokwa damu sana hivyo walilalamika maumivu," alidai shahidi na kuongeza:

"Majeruhi hao walitokea Kijiji cha Mpeta kwamba askari polisi walikuwa wakiwahamisha eneo lao la kilimo, niliwawekea maji ya dripu, nikawapa dawa za maumivu na za kutibu majeraha, lakini wakati nikiendelea na matibabu walikuja askari polisi baadhi nilikuwa nawafahamu wengine siwafahamu wakadai kwamba wamekuja kuwachukua wahalifu wamewaua askari wenzao wawili," alidai Dk. Kiluhungwa.

Aliwataja majeruhi hao kuwa ni, Kono Mwandu, Shishi George na Jumanne Jackson na baada ya kuwapa matibabu aliwaacha wodini akarudi ofisini kuhudumia wagonjwa wengine.

Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa utendaji wake wa kazi ikitokea majeruhi amefikia hospitali anajimudu anaagizwa kwenda kuchukua fomu namba tatu na kwa hali ya majeruhi aliowapokea alilazimika kuwaagiza ndugu zake kwenda kuchukua fomu hiyo wakati akiendelea kuokoa maisha yao.

Aliendelea kudai kuwa hakuwaona tena wagonjwa hao na kwamba aliwasiliana na ndugu wa majeruhi hao ambao walimthibitishia kuwa ndugu zao wamepelekwa gerezani Kigoma na wako hai.

Upande wa utetezi uliongozwa na wakili, Getrude Beneth.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili wa utetezi na shahidi:

Wakili: Shahidi umesema uliambiwa wale watu wako hai ulijiridhisha vipi?

Shahidi: Sikuwa na uhakika kama wako hai au la kwa sababu sikuwaona.

Wakili: Tukisema kuwa wamefariki tutakuwa tunakosea?

Shahidi: Mimi sijui kama wamekufa au la.

Wakili: Askari walipofika waliongea chochote kuhusu kuwapiga risasi?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Hali waliyokuwa nayo wangeweza kuruhusiwa kwenda nyumbani?

Shahidi: Hapana, ndiyo sababu niliwalaza wodini, Polisi waliwachukuwa wakiwa wodini wakati mimi nikiwahudumia wagonjwa wengine.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa unaomba tarehe nyingine ya kuita mashahidi wengine.

Hakimu Shaidi alisema kesi hiyo itaendelea kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri Agosti 13 na 14, mwaka huu.

Katika kesi ya msingi, Zitto anadaiwa kuwa Oktoba 28, 2018, Zitto akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika katika Makao Mkuu ya ofisi ya chama cha ACT-Wazalendo, alidaiwa kutoa maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

Inadaiwa alisema: "Watu ambao walikuwa ni majeruni katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika Kituo cha Afya Nguruka, Polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua".