KESI YA ZITTO Shahidi adai majeruhi walichukuliwa kuhojiwa

23Oct 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
KESI YA ZITTO Shahidi adai majeruhi walichukuliwa kuhojiwa

MKUU wa Upelelezi Mkoa wa Morogoro (RCO), Mrakibu wa Polisi, Albart Kitundu (49), amedai mahakamani katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, kwamba hakuna majeruhi aliyechukuliwa na Jeshi la Polisi kwenda kuuawa bali walichukuliwa hospitali na kwenda kuhojiwa ...

kuhusiana na tukio.

Kadhalika alidai kuwa aliwasiliana na RCO wa Kigoma kuhusu tukio hilo na alimweleza ukweli kuwa amewahoji watu mbalimbali na kuwa watu waliokufa kwenye tukio hilo ni wanne na si zaidi ya 100.

Ushahidi huo aliutoa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na jopo la Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, akisaidiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Nassoro Katuga na Colonel Tesha.

Akiongozwa na Katuga, shahidi huyo alidai kuwa Oktoba 28, 2018 alikaimu nafasi ya RCO Mkoa wa Kipolisi Kinondoni baada ya bosi wake kuwa na udhuru.

Pia alidai kupata taarifa kwamba viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo watafanya mkutano na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chama chao Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

"Nilijiridhisha kama wana kibali cha kufanya mkutano huo, nilibaini kwamba wanacho kibali," alidai shahidi.

Alidai kuwa aliteua makachero wawili kwenda kuhudhuria mkutano huo ili kuweka kumbukumbu zinazohitajika kama kielelezo katika jinai.

AlidaI waliporejea makachero aliowaagiza aliona picha za video walizorekodi kwenye mkutano huo wakati mshtakiwa akitoa kauli za uchochezi kwamba watu zaidi ya 100 wameuawa na Jeshi la Polisi kitongoji cha Mpeta, Wilaya Uvinza na waliokwenda kutibiwa katika zahanati ya Nguruka mkoani Kigoma.

Vile vile, alidai Oktoba 29, 2018 bosi wake RCO Malulu alipofika ofisini alimwita na kumfahamisha kwamba amekuta kundi la watu likijadili hotuba ya Kabwe na kwamba wamechukizwa sana na serikali ikiwamo Jeshi la Polisi.

"Bosi wangu alinipa kazi ya kufungua jalada la uchunguzi nikiongoza timu ya wapelelezi wenzangu wawili nilifungua jalada la uchunguzi, nilianza kupitia hotuba kupitia video iliyorekodiwa siku ya tukio," alidai na kuongeza:

"Kabwe alikamatwa nyumbani kwake na kuletwa ofisini kwangu nilizungumza naye kirafiki na baadaye nikamjulisha haki zake na kwamba nataka kuchukua maelezo yake kama mtuhumiwa, lakini alikataa na kudai atatoa maelezo yake mahakamani."

Akifafanua zaidi alidai kuwa aliwasiliana na RCO wa Kigoma akamweleza kwamba aliwahoji watu mbalimbali waliofahamu kuuawa watu wanne wakiwamo askari polisi wawili na raia wawili na si zaidi ya 100.

"Mheshimiwa hakimu, RCO Kigoma alieleza kwamba hakuna majeruhi waliochukuliwa hospitali na kupelekwa kuuawa na polisi bali walikwenda kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo," alidai SP Kitundu.

Akihojiwa na wakili wa utetezi Peter Kibatala, shahidi alidai kuwa hakumbuki kama kuna kifungu cha sheria kinachowataka viongozi wa siasa kuomba kibali cha kufanya mkutano na waandishi wa habari.

Alidai kuwa bosi wake aliamuru lifunguliwe jalada la uchunguzi baada ya kusikia maneno ya chuki dhidi ya serikali kutoka kwa wananchi.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri leo.

Katika kesi ya msingi, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi, anadaiwa kutenda makosa hayo, Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo.

Habari Kubwa