Kiama cha watoto wa vigogo bandari chaja

23Jun 2016
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Kiama cha watoto wa vigogo bandari chaja

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, ameitaka Bodi mpya ya Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kuondoa mtandao wa vigogo walioajiriwa bandarini bila kuwa na sifa, huku akisisitiza kuwa hata kama kuna mtoto wa kigogo yeyote yule, aondolewe.

waziri Makame Mbarawa

Profesa Mbarawa aliyasema hayo wakati akizindua Bodi mpya ya TPAjijini Dar es Salaam,

Alisema mbali na vigogo wa bandari hiyo kuajiri watu kwa kuzingatia undugu, hata wale waliokuwa wanapata zabuni mbalimbali bandarini walikuwa ni wafanyakazi wa chombo hicho ama ndugu zao.

Kutokana na hali hiyo, alisema bandari ilikuwa inatumika zaidi kuzalishia watu hao na ndugu zao badala ya kufanya kazi ya taifa.

“Nafahamu kwamba, kwa asilimia kubwa kampuni zinazofanya kazi bandarini ni za wafanyakazi wa bandari wenyewe na kama siyo wafanyakazi basi ni za ndugu zao.

“Hali hii ndiyo imefikisha bandari hapa ilipo kwa sababu pesa inayopatikana inaingia mifukoni mwao badala ya kukuza uchumi wa nchini, kwa hiyo ninaagiza mtandao wote huu uondolewe, hata kama ni Mtoto wa Mbarawa au wa DG (Mkurugenzi Mkuu wa Bandari) ama wa mkubwa yeyote, nataka wawekwe watu wenye sifa ambao watafanya kazi ya kuingizia nchi mapato,” alisema Mbarawa.

Mbali na agizo hilo, Profesa Mbarawa ameitaka bodi hiyo kuhakikisha inakuza mapato ya bandari na kila mwaka iwe inazalisha kuanzia Sh trilioni moja kwa mwaka tofauti na sasa ambapo inazalisha Sh bilioni 600.

Alisema endapo bodi hiyo itashindwa kufikia lengo hilo, ni vyema ikaondoka kwa kutumia mlango iliyoingilia.

“Nyie wajumbe ndiyo wenye uwezo wa kuinua bandari au kuididimiza, tumewaamini tumewapa kazi ya kuifufua bandari, tunaomba mhakikishe mnalitekeleza hilo,” alisema.

Alitaka ihakikishe inakata matumizi yasiyokuwa ya lazima.

Mbali na suala hilo, alisema kuwa baadhi ya wafanyakazi waliokuwa bandarini wakaondolewa na kupelekwa wizarani, kwa sasa wanahaha kuhakikisha wanarudi kwenye chombo hicho.

Alisema wafanyakazi hao wanatembea kila kona wakigawa rushwa na kwamba, hata yeye mwenyewe wamemfuata mara kadhaa hata akiwa nje ya Dar es Salaam.

“Pamoja na kwamba hawa watu wana uwezo wa kifedha na wanaweza kununua hata bodi, lakini hawatarudi hapa, taarifa zao zote tunazo na ninawahakikisha kwamba zinafanyiwa kazi,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema watu waliotengeneza mifumo mibovu ya malipo bandarini ili waweze kujipatia fedha, wamebainika baada ya kamati iliyoundwa kuchunguza suala hilo kumaliza kazi yake.

“Ripoti hiyo tunayo na imeshawasilishwa wizarani, ina majina ya watu hao, naomba tume ikishakabidhiwa hiyo ripoti ihakikishe kwamba watu hao hawafanyi tena kazi bandarini, wapelekwe huko mikoani wakasaidie kujenga bandari, sitaki kusikia wanapewa barua ya onyo,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema baada ya bodi hiyo kupata taarifa hiyo, wahakikishe wanaitumia kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato ya bandari.

Alisema pia bodi hiyo ihakikishe kuwa bandari za Mtwara na Tanga, Mwanza na nyingine zote nchini zinafanya kazi kama inavyotakiwa.

Kuhusu vifaa vya upimaji mafuta bandarini (Oil flow metres), Profesa Mbarawa aliagiza bodi hiyo kuhakikisha zinaanza kufanya kazi mara moja kwa kuzitengeneza ama kununua nyingine.

“Sitaki kusikia kwamba zinaanza kufanya kazi ikifika miaka mitatu zimekufa kwa sababu uwezo wake wa kufanya kazi ni miaka 10,” alisema Profesa Mbarawa.

Alitaka pia bodi hiyo kuhakikisha bandari inafanya kazi kwa saa 24 siku saba za wiki tofauti na ambavyo kwa hivi sasa kwenye siku za mapumziko ya mwisho wa wiki (Jumamosi na Jumapili) haifanyi kazi.

Kuhusu mizigo kupungua bandarini, alisema tatizo kubwa ni bandari kutojitangaza tofauti na zinavyofanya bandari nyingine.

Alisema TPA inafanya kazi kizamani na haina kitengo kinachoweza kutangaza bandara za Tanzania ili kuvutia wasafirishaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi hiyo, Profesa Ignas Rubaratuka, alisema bodi hiyo itahakikisha nidhamu ya bandari nchini inarejea.

Habari Kubwa