Kiama wahalifu daftari la mpigakura

19Jul 2019
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Kiama wahalifu daftari la mpigakura

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema mpigakura atakayejiandikisha vituo zaidi ya kimoja na ikathibitika wakati huu wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura lililoanza jana katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, wajiandae kuchukuliwa hatua za kisheria.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura jana katika uwanja wa Mandela katika Manispaa ya Moshi. PICHA: GODFREY MUSHI

Pia, amezionya asasi zote za kiraia zilizopata vibali vya kutoa elimu ya mpigakura kutoa elimu hiyo kwa wananchi kwa kuzingatia mwongozo wa elimu ya mpigakura uliotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Majaliwa alitoa kauli hiyo jana katika Uwanja wa Mandela, Manispaa ya Moshi, wakati akizindua zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura lilioanza jana hadi Julai 24, mwaka huu mkoani Kilimanjaro.

Baada ya hapo uboreshaji utaendelea kwa siku saba katika maeneo mengine ya Tanzania Bara kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na NEC.

“Hakuna mtu atakayeachwa katika kujiandikisha na hakuna mtu atakayeruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 pasipo kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura na kuwa na kadi ya mpigakura.

“Lakini pia kama ambavyo wamesema ‘wana msanja’ (kikundi cha utamaduni wa ngoma za asili), hairuhusiwi kujiandikisha vituo zaidi ya kimoja na ikithibitika hivyo lile lile lililosemwa na msanii wa msanja, tuta…(wanamalizia wananchi wakisema, watasweka ndani).

Waziri Mkuu alieleza kuwa uboreshaji huo unafanyika wakati mwafaka kuwa maandalizi ya uchaguzi mkuu mwakani 2020 yamekaribia na kwamba serikali itaendelea kuiwezesha NEC ili kukamilisha uboreshaji wa awamu zote mbili kwa mujibu wa sheria.

“Leo (jana) tunaanza na tukishamaliza, tutafanya mapitio tena, wale ambao watakuwa wamesahauliwa, wale ambao walikuwa na dharura watapata fursa ya kujiandikisha. Na katika uandikishaji wewe mtendaji huna haja ya kujua anatoka chama gani ili mradi ni Mtanzania, yuko mbele yako mwandikishe ili aweze kutimiza haki yake, suala la chama atajua yeye mwenyewe.”

Aonya asasi za kiraia

“Nimeambiwa kuwa Tume imetoa vibali vya kutoa elimu ya mpigakura kwa baadhi ya asasi za kiraia, rai yangu kwa asasi zote za kiraia zilizopata vibali hivyo kuendelea kutoa elimu hiyo kwa wananchi kwa kuzingatia mwongozo wa elimu ya mpigakura iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, na wala msijihusishe kukisemea chama chochote, elezeni umuhimu wa kujiandikisha, umuhimu wa kupiga kura, umuhimu wa kupata kiongozi uliyemchagua.”

Tahadhari ya Waziri Mkuu, Majaliwa, kuhusu watakaojiandikisha zaidi ya kituo kimoja ilitokana na tungo za wimbo wa hamasa ulioimbwa na kiongozi wa kikundi cha utamaduni wa ngoma za asili aitwate ‘Biusi’ kabla ya hotuba yake.

Tungo hiyo ilikuwa na maneno yanayoeleza kuwa kuna watu wanadanganywa njoo jiandikishe hapa na pale, utapiga kura tu, twakuomba Waziri Mkuu, watu watakaojiandikisha zaidi ya mara moja waswekwe ndani.

Mwenyekiti NEC

Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Semistocles Kaijage, alisema tume katika kujiandaa na uboreshaji wa daftari, iliendesha zoezi la uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapigakura nchi nzima, zoezi ambalo lilifanyika mwaka jana.

Jaji Kaijage alisema, lengo lake lilikuwa ni kuona kama vituo hivyo bado vipo na kama bado vina hadhi ya kuwa vituo vya kuandikisha wapigakura kwa mujibu wa sheria.

“Na vile vile kuangalia iwapo kuna maeneo yanayohitaji kuongezewa vituo, kwa upande wa Tanzania Bara, tume iliongeza vituo vya kuandikisha wapiga kura kutoka 36,549 hadi 37,407, vituo 6,208 vimebadilishwa majina, vituo 817 vimehamishwa kutoka kijiji au mtaa mmoja kwenda mwingine na vituo 19 vimehamishwa kutoka kata moja kwenda kata nyingine,” alisema.

Kwa upande wa Tanzania Zanzibar, Jaji Kaijage alisema tume imeongeza vituo vya kuandikisha wapigakura kutoka vituo 380 hadi vituo 407.

Habari Kubwa