Kibali chakwamisha kesi ya Zitto

19Jun 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kibali chakwamisha kesi ya Zitto

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, umedai mahakamani unasubiri kibali cha Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu cha kuita mashahidi kutoka nje ya Dar es Salaam.

Kesi hiyo ilipangwa jana kuendelea kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri, lakini ilishindwa kuendelea kutokana na upande wa Jamhuri kuwa bado hawajapokea kibali cha kuita mashahidi kutoka mkoani Kigoma.

Madai hayo yalitolewa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi.

Katuga alidai kuwa mashahidi hao ni muhimu na kwamba Jamhuri inasubiri kibali hicho.

"Mheshimiwa tunaomba muda wa mwezi mmoja wakati tunasubiri kibali cha kuita mashahidi kutoka Kigoma. Mashahidi hao ni muhimu sana katika kesi hii," alidai Katuga.

Upande wa utetezi ulidai kuwa hauna pingamizi na ombi la Jamhuri.

Hakimu alisema kesi hiyo itasikilizwa siku mbili mfululizo Julai 16 na 17, mwaka huu na dhamana ya mshtakiwa inaendelea.

Awali aliposomewa maelezo ya awali, Zitto alikana kwamba Oktoba 28, mwaka jana katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT - Wazalendo kwa nia ya kuleta chuki miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la Polisi, alitoa maneno ya uchochezi.

Zitto alikana maneno ambayo anadaiwa kuyasema kuwa "Watu ambao walikuwa majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi, wakiwa wamekwenda hospitalini kupata matibabu katika Kituo cha Afya cha Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua.”

Jamhuri inadai maneno hayo yalikuwa ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

Mshtakiwa anadaiwa kutoa maneno kwamba: “Lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta Nguruka, Uvinza ni mbaya ni taarifa ambazo zinaonyesha wananchi wengi sana wameuawa na Jeshi la Polisi, pamoja na kwamba Afande Sirro amekwenda kule, halijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi....kama hawa Wanyantuzu walivamia eneo la ranchi, kuna taratibu za kisheria za kuchukua nasiyo kuwaua, wananchi wengi sana wamekufa.”

Inadaiwa Zitto katika mkutano huo huo alitoa waraka kwa umma ukiwa na maneno ya kichochezi kwa nia ya kuleta chuki kwa Watanzania dhidi ya polisi.

Habari Kubwa