Kibano chaja halmashauri mapato kiduchu

16May 2022
Ashton Balaigwa
MOROGORO
Nipashe
Kibano chaja halmashauri mapato kiduchu

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, inakusudia kuzichukulia hatua kali halmashauri na mikoa itakayoshindwa kufikia asilimia 80 ya makusanyo ya mapato ya ndani ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa fedha.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Abdallah Chaurembo, alisema juzi mkoani hapa wakati wa akipokea taarifa ya makusanyo ya mkoa kwenye ziara ya kamati hiyo ambayo iliyotembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali za Biashara za wanyonge Tanzania (MKURABITA).

 Chaurembo alizitaka halmashauri kuongeza juhudi mbalimbali zitakazowezesha usimamizi wa makusanyo ya fedha kwa kipindi cha mwezi mmoja, ili zitumike kwa maendeleo ya uchumi na huduma za kijamii.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi, alisema mbali na MKURABITA kuanzishwa kwa lengo la kuwapa nguvu ya kiuchumi wananchi kwa kuwaongezea uwezo wa kumiliki na kufanya biashara katika mfumo unaozingatia utawala na sheria, imekuwa ikifanya na taasisi mbalimbali za kifedha hapa nchini.

 Alisema MKURABITA inafanya kazi licha ya kazi zake baadhi kutoonekana wazi, akieleza namna mkoa wa Dodoma waendesha usafiri wa pipikipi walivyonufaika kupitia moja ya kufanyika mpango mkakati wa kuliwezesha kiuchumi kundi hilo.

Mtendaji Mkuu MKURABITA, Dk. Seraphia Mgembe, alisema mpango umetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo mbalimbali nchini ikiwamo Morogoro kwa kushirikiana na halmashauri za manispaa na wilaya ikiwamo utoaji mafunzo kwa wananchi, umiliki wa biashara na kuiendeleza miradi hiyo.

Pia alisema mpango huo umefanikiwa kutoa wazo la namna ya kukuza huduma ya usajili na utoaji wa leseni za biashara kwa halmashauri la kujengwa kwa vituo vya utoaji huduma za pamoja (One Stop Centre). 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela, alisema katika utekelezaji wa makusanyo mkoa huo una deni la asilimia 17, ili kufika asilimia 100 na kwamba wameweka mkakati wa kusimamia watendaji waliopewa jukumu la ukusanyaji ndani ya muda uliobaki.

Habari Kubwa