Kibano kwa shule binafsi chaja

13Jul 2020
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Kibano kwa shule binafsi chaja

SERIKALI imewaagiza wathibiti ubora wa shule, kufanya uhakiki na ukaguzi wa kina kwa shule binafsi kama zinaendelea kufuata miongozo inayokidhi vigezo vilivyowekwa.

Miongozi mwa vigezo hivyo ni kuwa na walimu wenye sifa na mikataba, majengo na kuwapo kwa bodi na kamati za shule na endapo zitabainika zina mapungufu hayo, zifungwe.

Agizo hilo lilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, wakati akifunga mafunzo kwa watumishi wapya wa udhibiti ubora wa shule nchini katika Chuo cha Ualimu Kigurunyembe mkoani hapa.

Alisema wapo baadhi ya wamiliki wa shule binafsi wamekuwa wakikiuka maagizo na miongozi ya uendeshaji wa shule hizo kutokana na dharau na ujeuri wa pesa, hali ambayo wakati mwingine inasababisha kushindwa kutoa elimu iliyokusudiwa huku lawama zikiangukia serikali.

“Wapo baadhi ya wamiliki wa shule binafsi wanaleta dharau kwa serikali kwa sababu wamejenga majengo yao…wao wana majengo, lakini wajitambue kuwa majengo ni mali yao na shule ni mali ya serikali hivyo wanapaswa kufuata taratibu zote zilizowekwa ikiwamo kuwa na kamati na bodi za shule pamoja na walimu wenye sifa,” alisema.

Alisema hatua ya kupitia shule hizo na kuona kama bado zinakidhi vigezo ni kutaka kusaidia watambue nafasi zao katika kuhakikisha wanatoa elimu iliyo bora na yenye kukidhi viwango vinavyokubalika ili kutatua changamoto ya elimu nchini.

Hata hivyo Dk. Akwilapo aliwaonya wadhibiti ubora kutojihusisha na vitendo vya rushwa kwa nia ya kuzikingia kifua shule hizo binafsi na badala yake atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo hatua kali zitachukuliwe ikiwamo kufukuzwa kazi.

“Hii ni serikali inayopiga vita kwa nguvu vitendo vya rushwa…yeyote yule kati yenu wadhibiti ubora atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo katika ukaguzi hatutasita kuchukua hatua kali dhidi yake ikiwamo kuondolewa kazini.”

Alisema idara hiyo ni miongoni mwa idara zinazotajwa kujihusisha na vitendo vya rushwa hasa wanapofanya ukaguzi katika shule zinazomilikiwa na sekta binafsi, hivyo kuhakikisha wanafanya kazi yao kwa kuzingatia maadili na viapo vyao.

Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Avemaria Semakafu, alisisitiza umuhimu wa wadhibiti ubora kuzingatia mavazi yenye maadili kwa utumishi wa umma pamoja na kufuata miongozi wakati wa kutekeleza majukumu yao kwa kuwa wao ni watu muhimu katika maendeleo ya elimu nchini.

Aliwataka watumishi hao kuzingatia suala la utunzaji wa kumbukumbu pamoja na nyaraka za serikali kuacha kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii, na atakayebainika kufanya hivyo sheria itachukua mkondo wake.

Habari Kubwa