Kibondo waomba kupatiwa vifaa vya upimaji UVIKO-19

14Oct 2021
Adela Madyane
Kibondo
Nipashe
Kibondo waomba kupatiwa vifaa vya upimaji UVIKO-19

DIWANI wa Mabamba, Shedrack Butobuto, katika wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, ameiomba serikali kuwapatia vifaa vya kupima ugonjwa wa UVIKO-19, ili kunusuru afya za wakazi wa kata hiyo.

Amesema kata hiyo yenye vijiji vinne vya Nyakasanda, Mabamba, Mkalazi na Nyange, imepakana na nchi jirani ya Burundi kwa takribani kilomIta 10 upande wa kijiji cha Mkalazi na Nyakasanda hali inayosababisha muingiliano wa moja kwa moja hasa katika shughuli za kilimo na biashara kupitia soko la ujirani mwema lililopo kijiji hapo.

“Kuna siku mbili za soko kwa wiki katika soko la ujirani mwema la Mkalazi, linalosababisha muingiliano wa wanachi wa Tanzania pamoja na Burundi, kwa siku moja ya soko tunapokea wakazi wa Burundi kati ya 300 hadi 500 ambao hupita kwa njia halali au njia za panya, na hakuna kipimo cha UVIKO -19, itakuwa vizuri kama tutapata vipimo hivyo ili kudhibiti ugonjwa huo kwa pande zote mbili," amesema Butobuto.

Butobo amewaomba wananchi wasiokuwa na elimu sahihi kuhusu chanjo ya UVIKO -19 wasiendelee kutoa taarifa ambazo siyo sahihi kwani zinawafanya walio na hiari ya kuchanja kushindwa kuchanja.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mabamba, Stanslaus Kilomba, amesema ili kuwatambua raia waliokwisha kupata chanjo viongozi wa serikali za Tanzania na Burundi wanapaswa kuwasiliana kwa karibu ili kuzuia maambukizi yasiyo ya lazima ya UVIKO- 19.

“Viongozi wa nchi hizi mbili wawasiliane kwakuwa utaratibu wa chanjo upo kwa nchi zote basi raia wake watembee na kadi za chanjo, itakuwa njia bora ya kudhibiti ambao hawajachanja waweze kujikinga na njia nyingine za kudhibiti ugonjwa huu, japo wote lazima tuendelee kujikinga,” amesema Kilomba.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Afsa Ibrahimu, amesema kutokana na mwingiliano wa wa raia wa nchi hizo mbili, serikali haina budi kufuatilia mwenendo wa chanjo ili kuhakikisha wananchi wote wananchanja ili kuwalinda na ugonjwa huo.