Kibong'oto kuanza kupima Ebola

27Jan 2020
Mary Geofrey
SIHA
Nipashe
Kibong'oto kuanza kupima Ebola

HOSPITALI ya Magonjwa ya Kuambukiza ya Kibong'oto wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro, inajenga maabara ya kisasa ya magonjwa ambukizi itakayofanya uchunguzi wa kina wa maambukizi ya virusi vikiwamo ya Ebola.

Kaimu Mkurugenzi wa Hospitalu ya Kibong'oto, Dk. Donatus Tsere, akifafanua jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Kukamalika kwa ujenzi huo kutarahisisha utoaji huduma katika Kanda ya Kaskazini badala ya kupeleka Sampuli kwenye maabara ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MHN).

Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Donatus Tsere, ameyaeleza hayo  mkoani humo, wakati akizungumza na waandishi wa habari, katika muendelezo wa ziara ya maofisa mawasiliano wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, katika kampeni maalum ya 'Tumeboresha Sekta ya Afya'.

Lengo la kampeni hiyo ni kuangazia mafanikio ya miaka minne ya Serikali katika sekta ya afya.

Anasema ujenzi wa maabara hiyo unatarajiwa kukamilika mwakani na kwamba itakuwa kubwa na ya kwanza kuwapo kanda ya Kaskazini ya daraja la tatu ijulikanayo kitaalamu kama Biosafety Level III.

Ujenzi ukiendelea katika maabara ya mpya ya kupima visuri vya magonjwa ya kuambikiza ukiwamo ugonjwa wa Ebola.

"Jengo la maabara hii litakuwa la ghorofa tatu na itakuwa na mtambo wa kisasa wenye uwezo wa kupima virusi kwa uwezo wa daraja la tatu bila kutegemea tena kwenda kupima MNH kama tunavyofanya sasa. Pia itakuwa na uwezo wa kupima virusi bila kuwa na tahadhari kubwa ya kupata maambukizi," anasema Dk.Tsere.

Anasema maabara hiyo itapima virusi vyote vya magonjwa ya kuambukiza na kuwa na uwezo wa kubaini virusi kwa madaraja ikiwamo Ebola ambayo kwa sasa hatuna mtambo wa kubaini virusi vyake.

Anasema gharama zote za ujenzi wa maabara hiyo ni Sh. bilioni 8 na tayari awamu ya kwanza ya ujenzi huo umekamilika, bado awamu ya pili ambayo pindi itakapoanza utakamilika ndani ya miezi saba.

Akizungumzia kuhusu ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) anasema asilimia kubwa ya wagonjwa wanatoka katika mgodi wa Mererani mkoani Manyara.

Anasema kati ya watu 100,000 waliopo mgodini  14,000 wanaugua TB na kwamba sababu za kuwapo kwa idadi kubwa na mazingira ya kufanyia kazi kuwapo na hewa nzito na vumbi.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo hospitali inatoa elimu ya kujikinga kwa wafanyakazi wa migodini na pia wamenunua mashine za kisasa kubaini wagonjwa wakiwa katika hatua za awali na kupata majibu kwa muda mfupi.

Dk.Tsere anasema wanatoa huduma za upimaji katika mgodi huo na wagonjwa wanaobainika kuwa na maambukizi wanawahi kuwapa matibabu ili kuepuka kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.

Anasema pia wameboresha huduma za matibabu kwa wagonjwa wa TB hivyo kufanya idadi ya wagonjwa wanaotibiwa kuongezeka kutoka 150 mwaka 2015 hadi sasa wagonjwa 180.

Anasema Serikali imesaidia nchini kote kuwa na vituo 145 vya kutolea huduma za upimaji wa TB hali inayofanya kuwapo na muamko wa wagonjwa kujitokeza kupata matibabu.

Habari Kubwa