Kicheko mabasi kusafiri usiku

11Jul 2019
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Kicheko mabasi kusafiri usiku

CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), kilielezea kufurahishwa na hatua ya serikali kusikia kilio chao cha miaka mitatu na kuruhusu mabasi kusafiri kwa saa 24.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, alisema uamuzi huo unakwenda kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya uchunguzi.

"Tunampongeza sana Waziri (wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola), kwa kuwa tumekuwa na maombi ya muda mrefu sana lakini sasa ametusikiliza na sasa usafiri unakwenda kuanza kwenye njia mbili. Ameonyesha ni waziri anayesikiliza watu na kujali kile tulichokililia muda mrefu," alisema.

Hata hivyo, alisema ni vyema serikali ikashirikiana na wamiliki kuwadhibiti madereva wa mabasi na malori ambao wanatumia vilevi na kuendesha magari.

"Tungependekeza kwenye mizani kuwe na vifaa vya kupima vilevi kwa madereva wote kwa kuwa dereva wa basi anaweza kuwa hajanywa lakini wa lori akawa amelewa. Hii itasaidia kuwadhibiti ingawa nasi tunawaelimisha madereva wetu kuwa makini na kuacha kutumia vilevi," alibainisha.

Kwa mujibu wa Mrutu, kuna mambo yamebaki ambayo ni kurundikwa kwa muda mrefu kwa faini za madereva na kuwa mzigo kwa wamiliki pamoja na kuwapo kwa vituo vingi vya ukaguzi.

"Mfano dereva anakaguliwa Kibaha, Chalinze na Morogoro na analazimishwa kuingia kwenye vituo vya mabasi na kulipa ushuru wakati hapakii wala kushusha abiria kwenye maeneo hayo. Tunaomba watuondolee kero hii," alisema.

Pia aliwataka wamiliki wa mabasi kuhakikisha wanakuwa na madereva wawili kwa kila basi ili kuhakikisha wanapokezana na kusafiri kwa umakini zaidi na kwamba wanaongea na madereva wao kuwa makini kwa kuwa usiku kuna malori mengi yanayosafiri.

Mrutu alisema suala la ving'amuzi kwenye mabasi ni jambo jema kwa kuwa wamiliki wanalala kwa utulivu na wanafuatilia kwenye mtandao kuona mwendo wa mabasi yao kwa kuwa hawaruhusiwi kutembea zaidi kilomita 80 kwa saa.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, alitangaza kuanza kwa safari za mabasi kwa saa 24 kwa njia za Dar kwenda Mwanza na Dar kwenda Musoma.

WASAFIRI WACHEKELEA

Umoja wa Haki za Wasafiri wa Barabara, Maji, Anga na Reli (Uhawata), umeipongeza serikali kwa kuruhusu mabasi kutembea kwa saa 24 kwa kuwa itapunguza usumbufu kwa abiria wa kulala kwenye mabasi.

Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Umoja huo, Francis Mugasa, aliiambia Nipashe jana kuwa kwa miaka miwili mfululizo alikuwa akitetea haki za wasafiri likiwamo suala la mabasi yanayokwenda mikoa ya mbali kutembea kwa saa 24.

"Nilishaandika sababu 11 za kwa nini mabasi yaruhusiwe kutembea kwa saa 24, niliikabidhi hadi kwa Waziri Lugola. Niipongeze tu serikali kwa kufanya uamuzi wa kuruhusu mabasi kutembea usiku," alisema.

Alitaja sababu za kutetea uamuzi huo ni kuwa abiria walikuwa wanalazimika kulala kwenye mabasi maeneo ambako hakuna usalama, kukosa huduma muhimu kama za choo na maji.

Alisema kusafiri kwa saa 24 kutarahisisha shughuli za wananchi, kuokoa muda wao na kuongeza kasi ya kukuza uchumi kupitia shughuli wanazofanya.

"Uchumi wa wananchi utaimarika kwa sababu mtu kukaa ndani ya basi siku mbili ni kumpunguzia muda wa kuzalisha kiuchumi kwa hiyo sasa hivi kama kusafiri siku moja ina maana wasafiri watakuwa na muda mzuri wa kutimiza malengo yao," alisema.

Kadhalika, aliishauri serikali kuwasimamia wamiliki katika utekelezaji wa jukumu hilo, kama kuna vyombo vya usafiri ambavyo haviwezi kusafiri kwa muda mrefu kuwapo na mabasi ya kubadilishana.

Aidha, aliishauri serikali kushirikiana na umoja huo katika kuhakikisha wanaboresha sekta ya usafiri nchini na kupunguza malalamiko.

POLISI YAONDOA HOFU
Wakati hali ikiwa hivyo, Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi kimewahakikishia abiria kuwa hakuna basi ambalo litaendeshwa kwa mwendo kasi.

Kamanda wa kikosi hicho, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Fortunatus Musilimu, aliiambia Nipashe jana kuwa wamejipanga kuhakikisha mabasi yanayosafiri saa 24 yanafika salama bila kusababisha ajali.

"Tunatekeleza maagizo ya waziri lakini pia tuna magari yetu ya doria ambayo hufanya doria usiku kucha. Wakati nyie mnalala sisi hatulali, tunazunguka usiku kucha. Hakuna shida magari yatafika salama, nawahakikishia usalama watumiaji wa vyombo vya usafiri," alisema Musilimu.

Imeandikwa na Salome Kitomari na Mary Geofrey.

Habari Kubwa