Kicheko wateja benki ya Twiga

07Nov 2016
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Kicheko wateja benki ya Twiga

BENKI ya Twiga Bancorp Limited inatarajia kuanza kufanya kazi kesho baada ya kukamilika kwa tathmini ya hali ya kifedha ya benki hiyo iliyofanywa na Benki Kuu (BoT).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na BoT, benki ya Twiga itaanza kutoa baadhi ya huduma za kibenki ikiwamo ukusanyaji wa marejesho ya mikopo ya wateja.

Hata hivyo, licha ya kuiruhusu kuanza kutoa huduma hiyo, BoT imeeleza kuwa bado iko katika mchakato wa kuchambua njia mbadala za kutatua tatizo la mtaji linaloikabili benki hiyo.

“Njia inayopewa kipaumbele ni kutafuta mtaji kutoka kwa wawekezaji wapya, mchakato utakaohitaji kuchambua hali halisi ya taarifa za hesabu za Twiga. Kazi hii inatarajia kuchukua takribani wiki tatu na itakapokamilika, Benki Kuu itaingia makubaliano na wawekezaji wapya kuhakikisha wanaingiza mtaji unaohitajika ili shughuli za kawaida za kibenki ziweze kuendelea,” ilisema taarifa hiyo.

Ilieleza zaidi kuwa benki hiyo itaendelea kuwa chini ya BoT hadi hapo utaratibu wa kuwamilikisha wawekezaji wapya utakapokamilika.

BoT ilitangaza kuiweka benki ya Twiga chini ya usimamizi wake tangu Oktoba 28, mwaka huu, baada ya kubainika kuwa na upungufu mkubwa wa mtaji.

Katika taarifa yake ya jana, BoT ilieleza kuwa itahakikisha inalinda maslahi ya wenye amana mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.

Ruhusa ya BoT kuendelea kwa shughuli za benki ya Twiga ni faraja kwa wateja zaidi ya 20,000 wa benki hiyo ambao kwa takribani wiki nzima tangu kuwekwa chini ya uangalizi, hawakuwa na uwezo wa kufanya miamala yoyote na hata kuchukua fedha kwa njia ya ATM.

Habari Kubwa