Kichocheo cha kasi ya matukio udhalilishaji wa kijinsia hiki

02Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Pemba
Nipashe
Kichocheo cha kasi ya matukio udhalilishaji wa kijinsia hiki

JUMUIYA ya Tumaini Jipya Pemba ‘Tujipe’ imesema rushwa muhali na mashahidi kutokwenda mahakamani kutoa ushahidi, ndio janga baya zaidi katika jamii.

Imeelezwa kuwa rushwa hiyo ni mbaya zaidi kuliko hata vitendo vya udhalilishaji.

Mratibu wa Jumuiya hiyo, Tatu Abdalla Mselem, alisema serikali kwa nia nzuri, ilizifanyia marekebisho sheria za ushahidi, sheria ya adhabu na ya mwenendo wa makosa ya jinai na kuweka adhabu kali kwa wakosaji, lakini hayo yote yanategemea jamii kutoa ushahidi.

Akizungumza kwenye mkutano wa masheha, waratibu wa wanawake na watoto wa shehia za Matale, Pujini, Uwandani, Mchanga Mrima na Wara Wilaya ya ChakeChake, wanasheria, watendaji wa kituo cha mkono kwa mkono na madawati, alisema, uwapo wa sheria kali ni jambo moja na utekelezaji ni jambo jingine.

Alisema, majaji, mahakimu, waendesha mashtaka, polisi na mawakili hawawezi kufanya jambo lolote ikiwa rushwa muhali itatawala katika jamili.

Aliwasisitiza masheha na waratibu wa shehia hizo, kuendelea kuwaelimisha wananchi na hasa waathirika wa matukio ya udhalilishaji ili wasiache kufika mahakamani kutao ushahidi na kukataa suluhu.

“Hapa lazima tujiulize sisi wanajamii tumekosea wapi, maana zamani ilikuwa tukilalamika adhabu ndogo kwa wakosaji… sasa kuna adhabu kali wanajamii hawafiki mahakamani kutoa ushahidi na wengine hupokea hata rushwa, jambo hili sio sahihi,’’ alieleza.

Katika hatua nyingine mratibu huyo alisema jumuiya yao imekuwa ikitafuta ufadhili kila kona kuhakikisha inaisaidia jamii ya Pemba katika kutokomeza vitendo vya udhalilishaji.

Hata hivyo, aliwasisitiza wanasheria wanaoendesha kesi za udhalilishaji, kuhakikisha wanazitumia sheria kama zilivyo ili wanaotiwa hatiani wasirudie kutenda makosa hayo.

Katibu wa Jumuiya hiyo, Ibrahim Omar Mohamed, alisema makosa ya udhalilishaji ni rahisi kutokomezwa Zanzibar ikiwa kila mmoja atatekeleza wajibu wake na rushwa kwake kuwa mwiko.

Alieleza kuwa iwapo jamii itaachana na rushwa muhali na kufika mahakamani kutoa ushahidi, na mahakimu na waendesha mashtaka kutimiza wajibu wao, matendo hayo yanaweza kuwa historia.

Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Pemba, Juma Ali Juma, akiwasilisha mada ya ukatili na unyanyasaji wa wanawake na watoto, alisema dawa ya kuyaondoa matendo hayo na jamii kutoa ushahidi mahakamani.

Sheha wa Shehia ya Matale, Mkubwa Hamad Hassan, alisema wakati umefika kwa vyombo vya sheria kuacha kukinzana kisheria juu ya aina ya adhabu kwa washtakiwa wa makosa hayo.

Naye Ofisa Mipango Wilaya ya Chakechake, Kassim Ali Omar, alisema changamoto zinapokuwa nyingi kuanzia ngazi ya jamii hadi kwenye utekelezaji wa sheria kwenye mahakama na polisi, inaipa shida jamii kuamini kuwa kuna siku matendo hayo yanaweza kuondoka.

Habari Kubwa