Kifusi chaua watu watatu

04May 2021
Allan lsack
Arumeru
Nipashe
Kifusi chaua watu watatu

WATU watatu wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya kufukiwa na kifusi katika machimbo ya changarawe, maarufu moramu, yaliyoko Kijiji cha Engorora wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Taarifa zilizothibitishwa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, zilibainisha kuwa watu hao walifukiwa na kifusi hicho jana asubuhi katika machimbo hayo wakati wakichimba changarawe.

“Ni kweli hilo tukio limetokea leo (jana) asubuhi majira ya saa tatu. Kulikuwa na wanakijiji sita wanachimba moramu na wakati wakiendelea na shughuli hiyo, kifusi kilianguka na watatu wakafa papo hapo.

“Wengine watatu walinusurika ingawa wameumia vibaya. Kazi ya kuwaokoa watu hao ilifanywa na wanakijiji wenzao na baada ya kuokolewa walikimbizwa kupata tiba ya awali, Zahanati ya Kisongo," alisema.

Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Nurdin Rajabu (29), Idd Hussein (26) na Bonkila Martine (27), wote wakazi wa Ngorbobo, Wilaya ya Arumeru.

"Ripoti ya awali niliyopokea inaonyesha kwamba waliojeruhiwa ni Evarist Martin (25), Haruna Mbasha (32), Elias Kigeso, wote wakazi wa Ngorbobo, Wilaya ya Arumeru," alibainisha.

Kwa mujibu wa Kamanda Masejo, miili ya watu hao watatu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru).

Vilevile, alisema majeruhi walipatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Kisongo na baada ya muda mfupi hali zao za kiafya ziliimarika na waliruhusika kurejea nyumbani.

RC KIMANTA

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Iddy Kimanta, ambaye alizuru eneo hilo la machimbo baada ya kutokea kwa ajali, alisema tayari ameelekeza maofisa madini kufanya upembuzi yakinifu kama machimbo hayo yanastahili kuendelea kufanya kazi au la.

"Huenda machimbo haya ya Engorora hayakuzingatia utaratibu wa kiusalama, lakini baada ya wataalamu kuyakagua, watatushauri nini kifanyike," alisema.

Habari Kubwa