Kigogo Halotel amwomba DPP yaishe

09Jul 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kigogo Halotel amwomba DPP yaishe

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeambiwa kwamba Mkurugenzi wa Halotel, Son Nguyen (46) na vigogo wengine watano wa Kampuni ya Viettel Tanzania, wameandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kwa ajili ya kukiri makosa yao 10.

Miongoni mwa makosa hayo ni la kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara zaidi ya Sh. bilioni 75.
Kesi hiyo ilipangwa kutajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Wakili wa utetezi Benedict Ishabakaki, alidai washtakiwa wamemwandikia DPP barua ya kuomba kukiri mashtaka yao.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa, na kwamba upelelezi wake bado haujakamilika, aliomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Wakili Ishabakaki, alidai wateja wake walishaandika barua kwa DPP, na kuwa wanaendelea na mazungumzo.

"Mheshimiwa Hakimu, washtakiwa wameandika barua kwenda ofisi ya DPP kwa ajili ya kukiri makosa yao, ambapo wanaendelea na mazungumzo, hivyo tunaomba tarehe fupi," alidai Ishabakaki.

Akijibu hoja hizo, Wakili Wankyo, alidai kwa kuwa wanaendelea na mazungumzo, ni wajibu wa wakili wa utetezi kufuatilia mazungumzo hayo yalikofikia na yakiwa tayari wataiambia Mahakama.

Hakimu Simba, baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, alisema mazungumzo yakikamilika kabla ya siku ambayo watapangiwa kuletwa itatolewa hati ya kuletwa washtakiwa hao mahakamani.

Kesi iliahirishwa hadi Julai 22, mwaka huu kwa kutajwa na washtakiwa walirudishwa rumande.

Mbali na Nguyen, washtakiwa wengine ni Nguyen Minh (40) na Vu Tiep, wote ni Mameneja wa Halotel, Ha Than (39) ambaye Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Halotel, Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni hiyo, Nguyen Cong na Kampuni ya Viattel.

Wanadaiwa kutenda kosa kati ya Juni 8, mwaka 2017 na Machi 26, mwaka huu maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambapo waliongoza genge la uhalifu ili kujipatia faida.

Ilidaiwa kati ya Juni 8, mwaka 2017 na Machi 26, mwaka huu maeneo ya Mikocheni, Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi kwa pamoja walitumia masafa ya redio bila kupata kibali kutoka TCRA.

Pia alidai kati ya Julai 7, mwaka 2016 na Machi 26, mwaka huu maeneo hayo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Vietnam kwa pamoja walitengeneza mfumo ambao ulitumia huduma za mawasiliano zinazojulikana kama Virtual Private Network (VPN) kinyume na taratibu.

Katika shtaka la nne, inadaiwa washtakiwa hao walikwepa kulipa kodi kwa TCRA kwa kutumia mitambo ya mawasiliano yaliyounganisha Viettel Tanzania na Vietnam kinyume na sheria.

Vile vile Juni 8, mwaka 2017 na Machi 26, mwaka huu maeneo hayo kwa kutumia masafa ya redio bila kupata kibali cha TCRA walisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh. bilioni 75.

Pia wanadaiwa kati ya Julai 7, mwaka 2016 na Machi 26, mwaka huu kwa kutumia mitambo ya VPN waliisababishia TCRA hasara ya Sh. bilioni 3.03.

Katika mashtaka saba washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Sh. bilioni 3.03 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya kuongoza genge la uhalifu.

Kampuni ya Viettel Tanzania inadaiwa kati ya Julai 7, mwaka 2016 na Machi 26, mwaka huu ilitakatisha Sh. bilioni 3.03 na mashtaka ya tisa na 10, washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Sh. bilioni 75 wakati wakijua fedha hizo ni zao la uhalifu.

Habari Kubwa