Kigogo kesi ya Escrow aachiwa

03Nov 2017
Hellen Mwango
Nipashe
Kigogo kesi ya Escrow aachiwa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi  Kisutu, Dar es Salaam imemwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma,-

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma.

Dhidi ya tuhuma za kupokea rushwa ya Sh. milioni 323 kutoka kwa mfanyabiashara James Rugemalira, ambazo ni sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Esrow.

Mjunangoma aliachiwa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Swai ulidai Kuwa unaomba kuondoa kesi hiyo mahakamani chini ya kifungu cha 98 (a) cha Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA).

"Mheshimiwa tunaomba kuiondoa kesi hii kwa sababu upande wa Jamhuri hatuna nia ya kuendelea nayo,"  alidai Swai.

Hakimu alisema kwa kuwa upande wa Jamhuri umeomba kuondoa kesi hiyo mahakama yake haina pingamizi imekubali ombi hilo chini ya kifungu hicho, hivyo kumwachia huru mshtakiwa.

Mapema Januari 14, 2015 Rugonzibwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka ya kupokea fedha za rushwa.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa alipokea rushwa ya Sh. milioni 323 kutoka kwa Rugemalira, fedha ambazo ni sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Esrow.

Ilidaiwa alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Rugemalira, ambaye alikuwa mshauri huru wa kitaalamu, Mkurugenzi Mtendaji wa VIP Engineering na mkurugenzi wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL0) kama tuzo kwa kushughulikia mambo ya ufilisi wa muda wa kampuni hiyo.

Habari Kubwa