Kigogo Takukuru aomba kesi kusikilizwa haraka

13Nov 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kigogo Takukuru aomba kesi kusikilizwa haraka

UPANDE wa utetezi wa kesi inayomkabili Mkurugenzi wa zamani wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kulthum Mansoor, umeiomba mahakama kuisikiliza haraka kesi hiyo.

Wakili wa utetezi, Elia Mwingira, ameiomba mahakama itoe amri ya kusikiliza kesi hiyo haraka ili mshtakiwa apate haki yake kwa wakati kwa sababu yupo ndani kwa muda mrefu.

Mwingira, pia alidai mteja wake anayekabiliwa na kesi ya kutakatisha Sh. bilioni 1.477, aliandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), na kwamba mazungumzo hayana mwelekeo mzuri.

Hata hivyo, upande wa Jamhuri umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Kesi hiyo ilipangwa kutajwa jana mbele ya Hakimu Mwandamizi Mfawidhi, Kevin Mhina katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wake haujakamilika.

Wakili Wankyo alidai wataelekeza wapelelezi kuhakikisha wanakamilisha upelelezi katika maeneo yaliyobaki.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mhina aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 26, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Mansoor anakabiliwa na mashtaka manane ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha Sh. bilioni 1.477.

Inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 2013 na Mei 2018, mshtakiwa alighushi barua ya ofa ya Agosti 13, 2003 kwa madhumuni ya kuonyesha barua hiyo imetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo huku akijua kuwa sio kweli.

Katika shtaka la pili, inadaiwa kati ya Januari 2012 na Mei 2017 maeneo ya Upanga ndani ya Wilaya ya Ilala, mshtakiwa kwa kudanganya alijipatia Sh. milioni 5.2 kutoka kwa Alex Mavika ambaye ni mtumishi wa Takukuru kama malipo ya kiwanja kilichopo Kijiji cha Ukuni Bagamoyo.

Pia inadaiwa kati ya tarehe hizo, Mansoor alijipatia Sh. milioni tatu kutoka kwa Wakati Katondo kama malipo ya kiwanja kilichopo maeneo ya Kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Mshtakiwa huyo pia inadaiwa alijipatia Sh. milioni tano kutoka kwa Ofisa wa Takukuru, Gogo Migutah kama malipo ya kiwanja kilichopo eneo hilo hilo.

Katika shtaka ya tano, inadaiwa Mansoor alijipatia Sh. milioni saba kutoka kwa Ekwabi Majungu, ofisa wa Takukuru kama malipo ya kiwanja hicho.

Mansoor anadaiwa kati ya Januari 2012 na Mei 2017, maeneo ya Upanga jijini Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini alijipatia Sh. milioni saba kutoka kwa John Sangwa kama malipo ya kiwanja cha eneo hilo.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa akiwa mwajiriwa wa Takukuru, alijipatia Sh. milioni tano kutoka kwa Rose Shingela kwa ajili ya malipo hayo.

Katika mashtaka ya utakatishaji fedha, inadaiwa kati ya Januari 2013 na Mei 2018 katika maeneo ya Upanga, mshtakiwa alijipatia Sh. 1,477,243,000 wakati akijua fedha hizo ni haramu na ni zao la kosa tangulizi la kughushi.

Habari Kubwa