Kigogo TANESCO kortini madai ya uhujumu uchumi

20Feb 2021
Halima Ikunji
Tabora
Nipashe
Kigogo TANESCO kortini madai ya uhujumu uchumi

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tabora, imewapandisha kizimbani maofisa waandamizi wawili wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa mashtaka saba likiwamo uhujumu uchumi.

Walipandishwa kizimbani ni aliyekuwa meneja wa TANESCO  Mkoa wa Tabora,  Mohamed Abdallah,  na mhandisi wake,  Melkiad  Msigwa. Miongoni mwa mashtaka hayo ni kuisababishia serikali hasara ya Sh. milioni 60.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka jana katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora mbele ya Hakimu  Tausi Mongi.

Waendesha mashtaka, Matereus Maranda na Simon Mashingia, walidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa walitenda  makosa hayo kati ya  Desemba, 2015 na Novemba, 2018  ikiwamo kuendesha genge la uhalifu.

Walidai kuwa Msigwa alighushi risiti kuonyesha kuwa amenunua vifaa mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kituo cha kupozea umeme kwenye mizani ya Puge wilayani Nzega.

Maranda alidai kuwa kati ya  Mei 10, 2016 na Juni 23, 2016,  katika Manispaa ya Tabora, akiwa mtumishi wa TANESCO  Mkoa wa Tabora, alighushi  risiti zenye namba 08645 na  0078 kuonyesha kuwa ni nyaraka halali kwa ajili ya kununua vifaa vya umeme huku akijua si kweli.

Aliendelea kudai kuwa katika tarehe zisizojulikana mwaka 2016, Msigwa akiwa Manispaa ya Tabora kwenye ofisi za TANESCO, aliwasilisha nyaraka zilizoghushiwa kutoka Lesheya Investment Company Limited na Soko Electrical Traders  kuonyesha kwamba vifaa vilivyoorodheshwa kwenye risiti namba 08645 na 0078 vilinunuliwa na Sinohydro Corporation Limited na kwamba nyaraka hizo ni halali huku akijua si kweli.

Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa Abdallah kwa nyakati tofauti, kati ya Machi, 2016 na Mei, 2018,  akiwa Meneja wa TANESCO  Mkoa wa Tabora, alitumia madaraka yake vibaya na kufanya ununuzi katika mradi ujenzi wa usambazaji umeme kwenye mizani ya Puge kazi ambayo tayari iliidhinishwa na Wakala wa Barabara (TANROADS)  ifanywe na M/S Mawenjeni Electrical Contractor na kujipatia manufaa yasiyo halali ya Sh. 20,492,600.72.

Ilidaiwa kuwa washtakiwa  kwa pamoja na wanakabiliwa na  makosa saba yakiwamo ya  kuendesha genge la uhalifu kinyume cha aya ya  4 (1)  ya jedwali la kwanza pamoja na vifungu vya 57  (1)  na 60  (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200,  marejeo ya  mwaka 2019,  kughushi kinyume cha vifungu vya 333, 335  (a)  na 337  vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16,  marejeo ya 2019.

Washtakiwa wote wawili wamepelekwa rumande hadi Machi 4, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya aina hiyo ambayo imeangukia kwenye makosa ya uhujumu uchumi.

Habari Kubwa