Kigogo TBC amruka Tido

12May 2018
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kigogo TBC amruka Tido

MKURUGENZI Mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Clement Mshana, amedai mahakamani kwamba Mei 28, 2012 alishangaa kupokea taarifa ya usuluhishi kutoka Channel 2 Group Corporation (BV1) ya Uingereza kwa madai ya kuisababishia hasara.

MKURUGENZI Mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Clement Mshana.

Mshana alitoa madai hayo jana wakati akitoa ushahidi dhidi ya mtangulizi wake katika nafasi hiyo, Tido Mhando, anayekabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka ikiwamo kuisababishia serikali hasara ya Sh. Milioni 887.1.

Kigogo huyo ambaye ni shahidi wa tatu wa Jamhuri, alitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Leonard Swai, shahidi huyo alidai kuwa kampuni hiyo iliwaahidi kuwapatia kazi ya kuhamisha urushaji wa matangazo kutoka mfumo wa analogia kwenda digitali katika televisheni.

Mshana ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC mwaka 2011 hadi 2016 alidai kuwa alishangaa na kushtuka kwa sababu walipelekewa madai ya pesa nyingi na walipewa siku 28 kuwa lazima TBC iwe imejibu madai hayo.

Alidai kuwa aliwasiliana na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya TBC iwapo analifahamu suala hilo au waliwahi kutoa baraka kwa sababu ndio wasimamizi wakuu wa shirika.

Hata hivyo, alidai kuwa mwenyekiti wa bodi alieleza kwamba hakufahamu mkataba huo ulioingiwa kati ya Tido na Channel 2 Group Corporation (BV1).

"Mwenyekiti wa bodi alinielekeza niandike barua kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo labda analifahamu suala hilo...Wizara ya Habari, ilimwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuliangalia hilo suala na kutoa ushauri wa kisheria na maelekezo"alidai shahidi na kuongeza.

"Katika kumbukumbu zangu Wizara ilitoa maelekezo kwa bodi ya wakurugenzi ya TBC iitishe kikao cha kujadili na kutoa mapendekezo kwa sababu ilitaka kujua zaidi kuhusu mkataba huo...mbali na wizara na AG, Msajili wa Hazina naye alifahamishwa kwa sababu yeye ndiye amepewa dhamana na mali za shirika pamoja na Wizara ya Fedha ambayo ni mtoa fedha," alidai Mshana.

Alidai kuwa katika taarifa ya usuluhishi aliyoipokea, Channel 2 Group Corporation alidai kuwa TBC imewasababishia kukosa faida ambayo wangeipata iwapo wangewekeza katika kuhamisha urushaji wa matangazo ya televisheni kutoka mfumo wa analojia kwenda digital.

Aidha, bosi huyo wa zamani wa TBC aliomba mahakama kupokea nyaraka za mkataba unaodaiwa kuingiwa kati ya Tido na Channel 2 Group Corporation, mikataba ya nyongeza na barua mbalimbali zinazoonyesha uwepo wa Mawasiliano kati ya TBC, AG, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na michezo, Wizara ya Fedha na TCRA juu ya suala hilo na kuomba kuzitoa mahakamani kama vielelezo kwa upande wa Jamhuri katika kesi hiyo.

Wakili wa utetezi, Ramadhani Maleta hakuwa na pingamizi na Mahakama ikavipokea.

Kesi imeahirishwa hadi Mei 18,mwaka huu mashahidi wa upande wa Jamhuri wataendelea kutoa ushahidi dhidi ya Tido.

Katika kesi ya msingi ilidaiwa kuwa Juni 16, 2008, akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kutia saini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume cha  Sheria ya Ununuzi wa Umma na kuinufaisha BVl.

Katika shtaka la pili, Tido ilidaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, 2008 alipotia saini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.

Katika shtaka la tatu, ilidaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kutia saini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.

Katika shtaka la nne, ilidaiwa kuwa Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kutia saini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.

Katika shtaka la mwisho, ilidaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC hasara ya Sh.887,122,219.19.