Kigogo wa ACT adai kutekwa

26Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR
Nipashe
Kigogo wa ACT adai kutekwa

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, anadai kutekwa na watu wasiojulikana majira ya asubuhi jana, kisha kujitokeza baadaye na kueleza kilichomtokea.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, aliwataka wanaomshikilia Naibu Katibu Mkuu huyo kumwachia mara moja.

Maalim Seif ambaye ni mgombea urais wa Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo, alisema kitendo cha kutekwa kiongozi hakikubaliki wakati utaratibu wa kukamata mtu unaeleweka.

Aidha, alisema hawapo tayari kuvumilia vitendo vyovyote vya uonevu vinavyopangwa kufanywa dhidi yao.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Awadhi Juma Haji, alisema wamepokea taarifa za kutekwa kwa Naibu Katibu Mkuu huyo wa ACT-Wazalendo Zanzibar, na kwamba taarifa hizo wanazifanyia kazi baadaye watatoa taarifa rasmi.

Nassor Ahmed Mazrui, anadaiwa kuvamiwa na watu wasiojulikana mapema jana asubuhi maeneo ya Saateni, Wilaya ya Mjini, wakati akielekea ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

AFUNGUKA

Akizungumza baada ya kuachiwa katika mkutano wa hadhara wa kufungwa kwa kampeni za ACT-Wazalendo jana jioni, Mazrui Nassor ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya Maalim Seif, alisema:

“Ama kwa hakika ilikuwa ni siku ngumu kwangu, lakini nimevumilia kwa sababu ni ukombozi wa Wazanzibari.”

“Leo saa mbili kasoro robo asubuhi nilipokuwa natokea Mtoni kuja Vuga kwa ajili ya maandalizi ya mkutano huu, tulipofika kwenye daraja la Sateni, walitokea watu na gari aina ya Prado, wakatugonga kwa nguvu ikatupiga na daraja, ikiwa hatuwezi kwenda mbele wala hatuwezi kurudi nyuma.”

“Wakati huo kuna watu walishuka kwenye hilo gari lililotugonga, wakapiga bastola juu na wakapiga kwenye tairi ya gari yangu, mlango wa dereva ukafunguliwa, dereva akavutwa na kutupwa chini, nikawekewa bastola juu ya uso wangu na nikawekewa nyingine sita, nikabebwa hangahanga na kutupwa ndani ya gari na kufunikwa uso wote.”

“Nilifunikwa na kukabwa roho kisawasawa, kitambaa cha uso nimekifungua mwenye saa sita na nusu mchana nilipotupwa katika pori la Bweleo.

“Kila mtu lazima alaani vitendo viovu vya kuteka nyara Wazanzibari kwa sababu ni viovu, hizi ni siasa potofu.”

Habari Kubwa