Kigogo wa PAC ashtuka madudu ripoti ya CAG

24Apr 2022
Sanula Athanas
Dodoma
Nipashe Jumapili
Kigogo wa PAC ashtuka madudu ripoti ya CAG

​​​​​​​WAKATI ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2020/21 ikiendelea kuchambuliwa na wadau mbalimbali, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka, amebainisha kushtushwa na mwenendo wa fedha na amana zilizoko-

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka.

-kwenye benki za nje ya nchi.

Ripoti hiyo ya CAG iliwasilishwa bungeni jijini hapa Jumanne ya wiki iliyopita na hivyo kuwa wazi kwa umma kwa mujibu wa Katiba.

Katika mazungumzo mahususi na Nipashe jijini hapa jana, Kaboyoka alisema Ripoti ya CAG imeibua 'madudu' mengi na makubwa kwenye mashirika ya umma na taasisi za serikali.

Kigogo huyo wa PAC alipoulizwa na Nipashe kuhusu jambo kubwa zaidi lililomshtua katika ripoti hiyo, alilitaja kuwa ni kushindwa kurudisha fedha na amana zilizo kwenye akaunti za benki za nje ya nchi.

Alitolea mfano Shirika la Bima la Taifa ambalo alisema kwa zaidi ya miaka mitano limeshindwa kufanya miamala kwenye akaunti ya Dola za Marekani Na.11156195 yenye Dola za Marekani 309,800.86, sawa na Sh. milioni 712; na akaunti ya paundi ya Uingereza Na. 0954391 ambapo pesa zake hazikujulikani ni kiasi gani.

Kaboyoka ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), alisema akaunti zote hizo ziko katika Benki ya Lloyd jijini London.

"Pili, Shirika la Bandari linamiliki Amana za kudumu zenye thamani ya Sh. milioni 432 huko Benki ya Deutsch, Uholanzi. Haijulikani tarehe ya akaunti kuiva na pesa kulipwa, hivyo rahisi pesa hizo kuingia kwenye hatari ya kupotea," alisema.

Kaboyoka alisema CAG pia amefanya kazi ya ziada kuangalia maeneo mbalimbali yenye matumizi mabaya ya fedha za umma.

MUDA PAC, LAAC

"Ushauri wangu ni kwamba kamati zetu za PAC na LAAC (Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa) zitengewe muda mrefu wa kupitia na kujadili taarifa hii ya CAG ili tuweze kulishauri vizuri Bunge litoe maazimio yatakayokidhi kiu ya walipakodi.

"Kama kamati tajwa hapo juu hazitaweza kupitia sehemu kubwa ya Ripoti ya CAG, kazi aliyofanya hatutaitendea haki maana Bunge ndilo lenye wajibu wa kuisimamia na kuiwajibisha serkali," alisema.

Akizungumza na Nipashe kwenye viwanja vya Bunge jana mchana, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Japhet Hasunga, aliunga mkono hoja ya 'bosi' wake kwamba kamati hizo zinapaswa kutengewa muda mrefu zaidi wa kuichambua Ripoti ya CAG.

"Kamati zinapaswa kuichambua ripoti ya jumla kisha zianze kuchambua taarifa zilizopo kwenye ripoti za kisekta. Kwa utaratibu wa kamati kupewa wiki mbili kufanya kazi hii, itakuwa ngumu kuifanya kwa ufanisi," alisema.

Kwa mujibu wa CAG Charles Kichere, taarifa ya ukaguzi wake kwa mwaka 2020/21 ina ripoti 20 zikiwamo zinazohusu hesabu za: Serikali kuu; serikali za mitaa; ukaguzi wa ufanisi; miradi ya maendeleo; mifumo ya Tehama serikalini; mashirika ya umma; haki jinai; na ukaguzi maalum uliofanywa katika maeneo mbalimbali.

Habari Kubwa