Kigugumizi kinavyoweza kutibika

30Nov 2020
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Kigugumizi kinavyoweza kutibika
  • *Mtu anaweza kukipata ukubwani

"UKIWA na kigugumizi pengine unaweza ukakosa hata ajira au mchumba. Kuna siku ilinichukua sekunde 60 kumaliza kutamka sentensi moja," ni maneno ya mwathirika wa tatizo hilo, Ally Abdallah.

Binadamu huzaliwa na hali hiyo ambayo ina vikwazo mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Kigugumizi, Oktoba 22, kila mwaka, waathirika wa tatizo hilo wanasema kuwa mtu akiwa na hali hiyo anakutana na vikwazo vingi.

Neno kigugumizi linatokana na kitenzi 'kugugumia' kwa Kiingereza 'stuttering' maana yake ni shida kwa baadhi ya watu wakati wa kusema au kutamka maneno.

Bingwa wa Masikio, Pua na Koo, kitengo cha Matamshi na Lugha, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Rachel Mkumbo, anasema tatizo hilo huwaathiri zaidi watoto wa kiume kuliko wa kike, na hasa walio kwenye umri wa kuanza kuongea wa miaka miwili hadi sita.

ALIVYOPATA KIGUGUMIZI

Ally Abdallah ni mwanazuoni na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Mitindo Maalum ya Uzungumzaji Tanzania (CHAMMUTA).

Anasema aliamua kuanzisha chama hicho ili kutoa elimu kwa jamii kuhusu kigugumizi na kuondokana na unyanyapaa, dhana na imani potofu kwamba wenye tatizo hilo wana matatizo ya afya ya akili.

“Kwa bahati mbaya tupo kwenye dunia ambayo haina subira. Dunia inakwenda kasi, watu wenye kigugumizi tuna mazingira magumu sana, unazungumza na mtu ambaye hana subira hawataki kutuacha tumalize kuzungumza wanatukatisha,” anabainisha Ally.

Iliwahi kunikuta kwenye usaili nilipata kigugumizi, jambo ambalo linaweza kuwa sababu ya walio na kigugumzi kukosa ajira katika baadhi ya maeneo.

Anasema baada ya kuhitimu masomo ya chuo, na kuamua kuanzisha chama hicho mwaka jana, ambacho kina wanachama 25, kinajumuisha wazazi na walezi wenye watoto walio na kigugumizi, baada ya kubaini huathiriwa zaidi.

“Nilipata kigugumizi nilipokuwa na miaka mitano, baada ya kufiwa na baba yangu mzazi, mama yangu alinielezea. Nilikuwa katika chumba alichokuwa amelazwa baba yangu na kushuhudia akikata roho,” anasimulia Ally.

Kuna siku ilipita zaidi ya dakika moja bila kumaliza sentensi, ndipo nikaanza kutembea na kalamu muda wote na kuiweka pembeni ya sikio, ili nikihesabu sekunde kadha najua siyo hali ya kawaida, naamua kumwandikia ujumbe mtu kwenye karatasi badala ya kuzungumza.

Pamoja na kuwa na hali hiyo mama yake alikuwa na matarajio makubwa kutokana na kuwa ni mzaliwa wa kwanza kwenye familia ya baba ya watoto 15.

Anasema kuna wakati mama yake alitamani awe mzungumzaji mzuri na mtiririko mzuri kama vile Bill Clinton, rais wa zamani wa Marekani.

“Kuna wakati tulikuwa tunaangalia televisheni na mama, chaneli ya CNN, kipindi hicho Bill Clinton ni Rais wa Marekani, kama unavyojua Clinton alikuwa na ‘flow’ nzuri akitoa hotuba zake.

Mama aliniangalia akasema mwanangu huwezi kuwa kama Clinton. Nilimtazama sikumjibu, ila niliwaza huyu mama anawezaje kufikiri mimi kuwa kama rais wa Marekani na kigugumizi hiki.”

Ally alijipa moyo kuwa mama yake hajui kuwa yeye ni Bill Clinton akiwa darasani.
Tangu akiwa shuleni hakutaka kuwaonyesha walimu wala wanafunzi kuwa ana tatizo la kigugumizi jambo lililomfanya kujipanga kabla ya kuanza kuzungumza.

Aliificha hali yake hiyo, lakini wakati anamaliza shule alipewa muda azungumze.

“Hapo ndipo nilijulikana ila sikutaka kujificha tena, niliona nitakuwa siwatendei haki walio na hali kama yangu. Nilipopewa muda wa kuzungumza na kurudi nyumbani, nikamweleza mama yangu, alishangaa.”

Niliona bora hali ijulikane ili jamii ifahamu hali zetu,” anabainisha Ally.

ANAYOPITIA

Anasema pamoja na kuishi na hali hiyo kwa miongo kadhaa, hupatwa na hali ambayo haizoeleki.

“Ninapokuwa nimebanwa sana na kigugumizi huwa nakosa pumzi, ninapomaliza kuongea utaniona ninavyokuwa nimechoka, pumzi inakuwa imeisha.”

Tangu apate kigugumizi uzoefu wake shuleni hadi chuo kikuu na kulingana na utafiti mbalimbali aliousomea na kufanya uchunguzi wake binafsi, amebaini mambo kadhaa.

ALIYOBAINI

Anasema amebaini kuwa kuna masuala ya imani potofu, kunyanyapaliwa, tiba duni, na kufanya watu wenye tatizo hilo kuwa wapweke kulingana na jamii inavyowachukulia.
Mara nyingi kigugumizi kinarithiwa iwapo mmoja katika familia anacho.

Anasema baadhi ya utafiti, unaeleza kuna watoto ambao wanaiga kigugumizi kutoka kwa mzungumzaji, hasa kutokana na tabia ya kuiga kila kitu.

Mzazi au mlezi anapaswa kumtazama machoni mtoto na kumwongelesha haraka haraka ili kuacha kuiga.

Anasema utafiti mwingine unabainisha kuwa kuna kasoro ya ‘neurolojia’ (mfumo neva unaojumuisha uti wa mgongo, ubongo na mishipa ya fahamu) inayoweza kuwa sababu ya kigugumizi ambayo mhusika amezaliwa nayo au kupata mshtuko.

“Sehemu hii inaweza kuwa kweli, kwa mfano mimi baada ya baba kufariki, wiki chache mama aliona nimeanza kupata kigugumizi, yawezekana nilipata mshtuko,” anasema.

“Kwanza nilichelewa kuanza kuongea, niliongea nikiwa na miaka mitatu na nusu, baada hapo nilipofika miaka mitano kigugumizi kikaanza,” anabainisha.

UZOEFU

Ally anasema mtu mwenye kigugumizi unapoongea naye ni lazima umwangalie usoni ili aweze kujenga kujiamini.

“Ishara ni kwamba wakati tunazungumza ulikuwa unaniangalia machoni ukaacha kuniangalia sababu nimekwama kumalizia sentensi, ndio unanimaliza kabisa, cha msingi ni kuendeleza mawasiliano,” anasema.

Anasema, kuna siku alikuwa anazungumza na mtu, kigugumizi kikamshika kwa muda wa sekunde 60, inavyoonekana mtu huyo alikuwa na haraka na kufanya kitu ambacho hatakisahau… “Alitoa mkono wake na kuangalia saa yake, muda wote huo bado nimeshikwa na kigugumizi, ilipita muda sijamaliza neno, kitendo cha kuangalia saa nilijihisi namchelewesha, lakini si kwamba nilipenda. Watu wenye kigugumizi tunahitaji subira.”

Anasema jamii inahitaji kujengwa, kuelimishwa na kuwa na tabia ya kuwa na ustahimilivu kwa watu wenye kigugumizi.

MAAJABU

Mtu mwenye kigugumizi akifuata ‘melody’ (mpangilio wa sauti) ya muziki, kigugumizi hupotea.

Katika njia ambazo nazitumia kupunguza kigugumizi ni kutumia ‘tune’ (mdundo) inapunguza sana, na herufi inayonipa shida sana kutamka ni 'A' na kibaya zaidi majina yangu yanaanzia na 'A'.

Najitahidi ninapojitambulisha sianzi na 'A', huwa nasema jina langu ninaitwa...fulani fulani."

DAKIKA 20 ZA WASILISHO

Dudley ni mwanachama wa CHAMMUTA, anasema alipata kigugumizi akiwa na miaka minane na sasa umri wake ni miaka 28.

Katika maisha yake tatizo kubwa alilolipata akiwa shuleni na kutaniwa.

"Wanafunzi wenzangu katika darasa moja na mimi walinitania, lakini niliishi hivyo hivyo nikamaliza sekondari nikaenda chuo.”

Kigugumizi changu kina mtiririko na mara nyingine kinapotea kabisa na sababu sizijui nakumbuka kuna kipindi nikiwa kazini nilikuwa nafanya wasilisho ambalo bosi wangu alitakiwa alifanye, lakini alipata dharura.

Kitu cha dakika tano kilinichukua dakika 20, mtu ukiwa unafanya wasilisho wanaokusikiliza wanajua ni la muda fulani dakika tano au 10, ukitumia muda mwingi inawachosha.

Kigugumizi changu kilifanya niendelee kwa muda mrefu nikaona nawapotezea muda.

Anasema mama yake ana kigugumizi kidogo, sio kama chake ambacho anaona ni kikali zaidi na aliwahi kuongea akiwa mtoto kama watoto wengine, lakini alipotimiza miaka minane akaanza kushindwa kuongea moja kwa moja.

Hutumia mbinu mbalimbali ili kukiepuka kwa kutamka maneno tofauti ambayo yanamkwamisha.

“Ukiwa na kigugumizi watu wakakuambia vibaya muda mwingine utaona ni bora nisiongee na kuwa kimya, hii inakufanya uwe mkimya na kujitenga,” anafafanua Dudley.

YANAYOWAKWAZA

Ally anasema pamoja na kuikubali hali hiyo yapo mambo kwenye jamii na kwamba baadhi hudhani wenye kigugumizi ni wahalifu na wasahaulifu wa mambo, kutokana na tatizo lao.

Anasema changamoto kubwa inayowakumba ni pale mtu anapoamua kumalizia sentensi yake.
"Utakuna mara nyingi unapomuona mtu mwenye kigugumizi akikwama sentensi ni kama amesahau, sikweli, utakuta mtu anakumalizia sentensi.

“Hili suala linatukera, linavunja moyo, niache nimalize kuzungumza, si kwamba nimemaliza na unaweza kufikiria nataka niseme hivi kumbe sivyo, jamii isitusemee," anasema Ally na kuongeza.

“Unaponisemea kigugumizi huwa kinaongezeka zaidi unakuwa umenitoa kwenye mstari, pale mtu anapokusemea au kukuwekea maoni yake,” anasisitiza.

Anasema msikilizaji hutakiwa kumpa subira mwenye kigugumizi, na haichukui sekunde tatu hadi 30 ili kumalizia sentensi moja.

"Utakuta mtu anakwambia polepole zungumza, usiwe na haraka, najiona kumbe sipo sawa, kigugumizi ndio kitachanganya."

Pia, anasema baadhi ya maneno yanayotumiwa na vyombo vya habari, hujiona wao ni sehemu ya tatizo kwenye jamii.

"Utakuta kichwa cha habari kinasema 'Mkurugenzi apata kigugumizi akihojiwa...hii sentensi nikiiona mimi niliye na kigugumizi nafikiria kwamba kigugumizi ni tatizo, watu waongo, wasio waaminifu,” anabainisha.

“Au msanii anaimba ‘nilipata na kigugumizi nilipokutana na mtoto mkali…' ni tatizo kwetu."
Anasema alipobaini neno kigugumizi jamii inalichukulia kwa mtazamo hasi, wakati wanaunda CHAMMUTA, alifikiria kutotumia neno 'Chama cha wenye Kigugumizi' na badala yake kutumia mtindo maalum wa kuzungumza ili kubadili mtazamo.

Habari Kubwa