Kigwangalla azindua mpango wa kufunga mkanda wa GPS Tembo

14May 2019
Happy Severine
Meatu
Nipashe
Kigwangalla azindua mpango wa kufunga mkanda wa GPS Tembo

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Khamis Kigwangalla, amezindua utaratibu wa kuwafunga Tembo mikanda yenye  mawasiliano na satelite inayotumika kurusha taarifa za mahali walipo wanyama hao kwa wakati husika.

kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Simiyu ikiongozwa na mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka,pamoja na Waziri wa maliasili na utalii Khamis Kingwangala wakishuhudia tembo aliyekwisha fungwa na gps.

Katika uzinduzi huo, Dk. Kigwangalla amesema  vitendo vya ujangili vimepungua na badala yake wanyama hao wameendelea kuvamia makazi ya watu na ili kuondokana na changamoto hiyo, serikali imekuja na mpango wa kuwafungia mikanda maalumu ya kuwatambia mahali walipo.

 "Kutokana na vitendo vya ujangili kupungua kumeibuka na changamoto mpya ya wanyama hao kuvamia makazi ya watu, kama serikali lazima tujipange na tupambane na changamoto hiyo"  Amesema Dk. Kigwangalla.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kingwangala akimwangalia tembo mara baada ya kufungwa mkanda wa mawasiliano, katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Meatu Dk Joseph Chilongani.

Naye Ofisa Mtafiti wa Wanyamapori kutoka Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Dk. Emmanuel Masenga, amesema wataweka mikanda hiyo kwa tembo 18 katika pori la akiba la Maswa na Hifadhi ya Jamii ya Makao (WMA).

Dk Masenga amesema zoezi hilo litapunguza vitendo vya tembo kuvamia makazi ya watu na wataweza kuwaona kiurahisi pindi wanapovuka mipaka kwenda kwa wananchi.

Habari Kubwa