Kigwangalla akumbana na Faru ‘Vicky’ ndani ya kreta

24Feb 2020
Marc Nkwame
Ngorongoro
Nipashe
Kigwangalla akumbana na Faru ‘Vicky’ ndani ya kreta

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Khamis Kigwangalla, wikiendi alishuka ndani ya Bonde la Ngorongoro kukagua miundombinu iliyoharibiwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha eneo hilo.

Hata hivyo, wakati akiendelea kutembelea njia za kreta zilizoharibiwa kwa mafuriko, ghafla faru mwenye umri mkubwa kuliko wote duniani, ajulikanaye kama ‘Mama Vicky,’ akaibuka na kulazimisha msafara wa Waziri kusimama kwa muda ili kumshuhudia mnyama huyo adimu.

Pamoja na kuwa ndiye faru mwenye umri mkubwa kuliko wote kwa sasa, Faru Vicky pia ni moja ya wanyama wenye miili mikubwa sana kiasi cha kwamba akiwa mbali ni rahisi kudhani kuwa ni tembo.

Meneja wa Mahusiano katika Mamlaka ya Ngorongoro, Joyce Mgaya, aliongeza kuwa, Faru Vicky pia ana rangi nyeusi zaidi kuliko faru wengine ndio maana ni rahisi kumtambua hata akiwa mbali.

‘Faru Vicky,’ mwenye umri wa miaka 46 kwa sasa, anashika nafasi ya ‘marehemu,’ Faru Fausta aliyefariki Desemba mwaka jana, na ambaye alivunja rekodi ya kuwa faru mwenye umri mkubwa kuliko wote duniani. Yeye alikuwa na miaka 57 alipokufa.

Faru wanakadiriwa kufikisha umri wa miaka 35 mpaka 40 wakiwa porini na kuishi zaidi ya hapo wakiwa chini ya ulinzi maalum.

Faru mwingine mweusi na jike aliyeishi porini kama Fausta na aliyefahamika kwa umri wake mkubwa ni Solio, wa nchini Kenya ambaye hata hivyo, hajafikia umri wa ‘Vicky’ (49) na aliachwa mbali na Fausta (57), huyo Solio alikuwa akiishi Kenya na kufa akiwa na umri wa miaka 42 mwaka 2016.

Tanzania inadaiwa kuwa na idadi kubwa ya faru, wanyama ambao ni adimu na hatarini kutoweka duniani. Hata hivyo, namba halisi ya faru waliopo katika hifadhi za Maswa, Serengeti, Mkomazi (Kilimanjaro) na Ngorongoro huwa haitajwi kwa sababu za kiusalama.

Wakati huo huo, juhudi za kurekebisha sehemu za barabara zilizomo ndani ya kreta ya Ngorongoro zimeanza kuzaa matunda, kwani sasa barabara hizo zinapitika kwa asilimia kubwa.

“Kwa sasa hali ni nzuri na tumejiweka sawa kwa mvua zaidi zinazotarajiwa kushuka kipindi cha masika kitakachoanza mwishoni mwa mwezi ujao (Machi),” alisema Dk. Freddy Manongi, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Ngorongoro.

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Adolf Mkenda, pia alitembelea miundombinu ya hifadhi za Serengeti na Ngorongoro, baada ya kuibuka taarifa kwamba mvua imeziharibu vibaya barabara za maeneo hayo.

Habari Kubwa