Kigwangalla:Nyalandu aliishi kama malaika

14Nov 2017
Sanula Athanas
Nipashe
Kigwangalla:Nyalandu aliishi kama malaika

SIKU chache baada Lazaro Nyalandu kutangaza kujiuzulu ubunge na kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, amemvaa mbunge huyo wa zamani wa Singida Kaskazini akimtuhumu kwa kashfa mbalimbali na kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.

Dk. Kigwangalla ambaye hivi karibuni alipandishwa cheo na Rais John Magufuli kutoka Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, alitoa tuhuma hizo dhidi ya Nyalandu bungeni mjini hapa jana wakati wa mjadala wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2018/19 na Mwongozo wa Maandalizi ya Bajeti kwa mwaka ujao wa fedha.

Huku akiibua mvutano mkali bungeni kati yake na kambi ya upinzani, Dk. Kigwangalla alisema kuna haja Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi dhidi ya Nyalandu.

Alidai kuwa amebaini Waziri huyo wa zamani wa Maliasili na Utalii (Nyalandu) aliisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 32 ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake wizarani hapo.

Kabla ya kuporomosha tuhuma hizo nzito, Dk. Kigwangalla, ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Vijijini, alisema baadhi ya wabunge, wengi wakiwa wa upinzani, walisema wakati wa mjadala huo kwamba ameanza kazi kwa kufukua makaburi na ana muda mfupi wa kukaa wizarani hapo.

Alisema yeye si mahiri sana kwa ufukuaji wa makaburi lakini akasisitiza kuwa ukiwa waziri na ukawekwa katika wizara ambayo wiki ya kwanza tu hata hujaanza kazi kila mtu anasema umekalia kuti kavu ni lazima kabla hujaanza kazi uliyopewa lazima kwanza kusafisha nyumba yako.

Alisema amezingatia msingi huo kwa kuanza kwa mtindo huo wa kufukua makaburi mpaka pale mtandao wa watu wote waliopo kwenye wizara hiyo wakiwamo wanaoshiriki kwenye ujangili, hujuma na wanaotajwatajwa katika kashfa mbalimbali za rushwa utakapofutika.

"Tukimaliza kuing’oa hii mitandao, sasa tutaanza kazi kubwa tatu na za maana zaidi katika nchi yetu ya kuongeza idadi ya watalii na idadi ya vivutio na tutafanya hivyo kwa kuwekeza kwenye kanda nyingine kama kusini ili kuifungua korido ya kusini, na serikali imepata takribani Sh. milioni 300 (Sh. bilioni 735) kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa kuifungua kanda ya kusini kiutalii," alisema.

Dk. Kigwangalla alisema zaidi: "Naomba niseme sikusudii kufukua makaburi ya mawaziri wazuri waliopita katika wizara hii wakapata ajali mbalimbali za kisiasa kama kina (Ezekiel) Maige, (Balozi Hamis) Kagasheki, Profesa (Jumanne) Maghembe.

"Labda nianze kwa kuzungumzia waziri mmoja ambaye wenzetu hawa wa upinzani walimsema sana alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na huyu si mwingine bali ni ndugu Lazaro Nyalandu.

"Nataka niseme tu kwamba rafiki yangu Mheshimiwa (Joshua) Nassari alizungumza kwa mbwembwe nyingi sana hapa bungeni kwamba kama Dk. (Wilbroad) Slaa..." (Alikatishwa na sauti za wabunge waliopiga kelele).

Kutokana na kelele kuibuka mjengoni, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu aliyekuwa anaongoza kikao hicho, alilazimika kusimama kuwanyamazisha na kuwataka kuwa wavumilivu.

“Jamani tulieni, ebu tulieni! Wewe, mimi ndiye 'ninaye-control' (ninayedhibiti) Kiti, wewe (Pascal) Haonga, Haonga kaa kimya, kaa kimya, huwezi kubishana na Kiti, kama kuna kasoro kwa mtoa hoja, mimi ndiyo nitarekebisha siyo wewe. Kaa kimya, tulia... itapendeza ukitulia,” Zungu alisema na kumruhusu Dk. Kigwangalla kuendelea kuchangia.

Baada ya bunge kutulia, Dk. Kigwangalla alisema: "Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua ukiwa unaishi kwenye nyumba ya vioo usianzishe vita ya mawe, kuna wengine kwa wale mliokuja wapya mnatakiwa mjifunze mazingira ya humu ndani. Kuna watu wanaguswa na kuna wengine hawaguswi.

"Mimi ni katika watu wasioguswa na huwa sipendi upuuzi hata siku moja. Kwa hiyo, mtu anasema nimeanza kazi kwa kufukua makaburi, sitaki kuwakumbusha yaliyotokea huko nyuma lakini naomba niwape uhakika tu mimi huwa sichezewichezewi.

"Wanasema nimeanza kazi hii kwa kufukua makaburi na mimi nasema leo (jana) nafukua moja na ninaanza kufukua hilo moja kwa maelezo yaliyotolewa na wenzetu hawa upinzani. Kwenye bunge lililopita walisema ndugu Lazaro Nyalandu kazi yake ni kustarehe na warembo kwenye mahoteli ya kitalii, kutembea nchi za mbali huko ikiwamo Marekani.

"Wakasema alienda Marekani na Aunty Ezekiel, wakasema Lazaro anatumia helikopta za wawekezaji kwa shughuli zake binafsi za kisiasa na ndugu Nassari alisema kama Dk. Slaa angeshinda urais mwaka 2015 na akampa yeye uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa siku moja tu angeanza kushughulika na mawaziri wa ovyo kama Lazaro Nyalandu.

"Sasa mwenyekiti leo naelewa kwanini Nassari alikuwa sahihi, kwa sababu wakati Waziri Nyalandu akistarehe kwenye Hoteli ya Serena pale Dar es Salaam akitumia helikopta ya mwekezaji wa TGTS, mezani kwake… (akakatishwa na sauti ya wabunge kutoka upinzani ambao waliomba kumpa taarifa waziri huyo)".

Hata hivyo, Zungu aliikataa kutoa nafasi kwa wabunge hao ambao Nipashe haikuwaona kwa sura na kutambua majina yao.

"Kuna sauti mbili za wabunge 'nimeshazi-mark' (nimeshazikariri), kama mnataka kuharibiana, tuambiane mapema. Mimi hapa ni 'referee' (mwamuzi) siyo kocha, kama mlivyotulia hivyo hivyo mnapendeza, endeleeni kutulia.” Zungu alionya.

Baada ya onyo hilo kwa wabunge wa upinzani, Dk. Kigwangalla aliendelea kulieleza bunge kuwa Nyalandu alikuwa akivinjari Hoteli ya Serena na alikuwa akifanyia kazi zake za wizara kwenye hoteli hiyo na akapewa chumba cha kuishi hotelini hapo.

"Mezani kwake kulikuwa na tamko la serikali kuhusiana na tozo za ada za hoteli za kitalii, mahoteli ambayo yapo ndani ya Mbuga ya Serengeti," Kigwangalla alisema.

Kauli hiyo ilimwinua kitini na kuomba 'utaratibu' Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), ambaye alisema hoja iliyokuwapo mezani ni kujadili mpango hivyo waziri alipaswa ajibu hoja zilizoibuliwa katika mjadala huo badala ya kuzungumza mambo ya Nassari na Nyalandu.

Hata hivyo, Zungu alisimama na kusema: "Bobali unazo kanuni, nenda kasome Kanuni ya 68(10)."

Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016, kifungu cha 10 cha Kanuni ya 68 kinasema: "Uamuzi wa Spika kuhusu suala lolote la utaratibu utakuwa ni wa mwisho", hivyo Bobali hakuwa na namna nyingine zaidi ya kuketi kutii kanuni.

Dk. Kigwangalla, kabla ya kuendelea, alimgeukia mbunge huyo wa CUF kwa kumwambia "Bobali mimi mzoefu humu ndani, mimi sijibu hoja, mimi nachangia, mwenye kujibu hoja yule pale (Dk. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango), ndiyo maana nasema mimi sichezewi kwa sababu najua kanuni. Mwenyekiti naomba niendelee kuchangia".

"Ninachokisema ni kwamba wakati Nyalandu alifanya yote hayo, moja kama Waziri wa Maliasili na Utalii, kulikuwa kuna tozo ya hoteli iliyopendekezwa na Tanapa na gazeti likatengenezwa likisubiri saini ya waziri ili serikali ianze kuchaji tozo hiyo kwenye hoteli za kitalii na hilo lingeongeza mapato kwa mwaka huo wa 2014 tungeweza kukusanya Sh. bilioni 16.

"Lakini waziri yule hakusaini hiyo hadi anaondoka madarakani, maana yake ndugu Nyalandu aliikosesha serikali mapato ya takribani Sh. bilioni 32.

"Hiyo ni moja na ni jambo ambalo watu wa hoteli walipinga, serikali ikashtakiwa mahakamani na ikashinda. Kwa hivyo waziri alikuwa hana lolote lile la kuamua kwa kuwa kulikuwa na amri ya mahakama kuwa serikali iko sahihi ichaji tozo hiyo na hakusaini hadi anaondoka madarakani.

"Sasa mambo kama hayo Mwenyekiti, mimi ukiniambia nafukua makaburi mniache tu niendelee kufukua kwa sababu bila kuweka mambo sawa, bila kujua kwanini Nyalandu hakusaini, bila kujua alikuwa anashirikiana na kina nani na je, aliokuwa anashirikiana nao wapo au wameondoka, huwezi kufanya kazi yako vizuri na ndiyo maana hata mawaziri watakaowekwa pale wataendelea kutolewa tu, wataendelea kukalia kuti kavu."

Dk. Kigwangalla alisema hayuko tayari kukalia kuti kavu wizarani hapo kwa kuwa hata akikaa kwa miezi mitatu tu, atakuwa amezinyoosha sekta zote zilizo chini ya wizara hiyo.

Alisema jambo la pili ni uhusiano aliouita wa kutatanisha aliyokuwa nao Nyalandu na wawekezaji wa taasisi maarufu iitwayo Freedking Foundation ambayo alidai inamilikiwa na bilionea kutoka Marekani.

Alidai taasisi hiyo ilikuwa ina kampuni zinazofanya kazi za utalii nchini na bado zipo mpaka sasa.

"Moja inaitwa Mwiba Holding, nyingine Tanzania Game Trackers Safaris (TGTS), kampuni iliyopewa zaidi ya vitalu vitano ambavyo angepaswa kwa mujibu wa sheria maana yake hapo kuna mambo hayako sawa, na bado kampuni hii ipo inafanya kazi kwenye sekta hii, ukisema nisifukue makaburi utakuwa unanionea," Dk. Kigwangalla alisema.

"Ni lazima nijue kwanini walipewa vitalu zaidi ya vitano, kwanini wanaendelea kuwinda. Kampuni ya Mwiba Holding inawinda, inafanya kazi za kitalii lakini imekamatwa na nyara za serikali na hizi kampuni zote zinamilikiwa na mtu mmoja anaitwa Tom Freedking ambaye ni rafiki wa Nyalandu, na waziri huyu alikuwa akifanya kampeni za urais wakati ule na sisi tukijaribu kuomba ridhaa ya chama alikuwa akifanya kampeni zake akitumia helikopita ambayo inamilikiwa na huyu jamaa.

"Sasa katika mazingira kama haya, waziri 'GN' ya kusaini iko mezani kwake hakusaini halafu unakaa kwenye hoteli."

Kutokana na maneno hayo, Haonga alionekana kukosa uvumilivu na kuamua kusimama licha ya Zungu kutangaza awali kwamba hapokei tena taarifa kuhusu mchango wa Kigwangalla.

Haonga alisema: "Kama yote hayo alifanya Nyalandu akiwa waziri alipaswa awe ameshachukuliwa hatua kwa maana ya kupelekwa mahakamani muda mrefu na asingeweza kusubiri kuona amehama chama ndiyo mnakuja na maneno ambayo ni mepesi mepesi,
siasa nyepesi Mwenyekiti haziwezi kujenga taifa hili."

Zungu alikataa taarifa hiyo na kumruhusu Dk. Kigwangalla ambaye aliendelea kuchangia huku akieleza kuwa zama zinabadilika na uongozi pia unabadilika.

Alisema kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii kwa sasa kuna waziri ambaye anaweza kumchukulia hatua Nyalandu.

"Kama ndiyo kilio chako Haonga, mimi nitaagiza hapa Takukuru pamoja na Jeshi la Polisi wayasikilize haya ninayosema, wachukue 'hansard' (kumbukumbu za taarifa rasmi za bunge) wakafanye uchunguzi ili waweze kumchukulia Nyalandu hatua," alisema na kueleza zaidi:

"Wala hilo halisumbui kama hiyo ndiyo kiu yako kama mwananchi na mbunge. Nyalandu atafika mahakamani, mahakama bado zipo na jinai haifi hata miaka mia ipo tu. Kwa hiyo vyombo vinavyohusika vichukue hatua."

Waziri huyo alisema jambo la tatu ni vitalu vya uwindaji ambavyo alidai kuwa kabla ya Nyalandu vilikuwa vikitolewa kwa kampuni mbalimbali na muda wa kuwinda ulikuwa ni kipindi cha miezi mitatu tu kati ya Julai na Oktoba ili kuwapa nafasi wale wanyama kupumua na kuzaliana lakini... (akakatishwa tena na mbunge alishauri alipe bunge taarifa za Maige na Prof. Maghembe).

Akimjibu mbunge huyo, Dk. Kigwangalla alisema: "Hizo ni katika taarifa ambazo silazimiki kuzijibu kwa sababu hazina maana yoyote.

"Nyalandu alivyopewa tu kiti cha uwaziri wa Maliasili na Utalii alichokifanya bila huruma yoyote ile, bila uzalendo wowote ule, alianzisha mchakato wa kubadilisha... (akakatishwa na Zungu baada ya muda wake wa dakika 15 kuchangia kumalizika).

Oktoba 30, mwaka huu, Nyalandu alitangaza kuachia nafasi yake ya ubunge, kuihama CCM na kuomba kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokana na kile alichodai kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho tawala katika baadhi ya mambo, ikiwa ni pamoja na uzingatiaji wa misingi ya sheria, demokrasia na utawala bora.

Habari Kubwa