Kiingereza bado pasua kichwa darasa la nne

16Jan 2017
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Kiingereza bado pasua kichwa darasa la nne

SOMO la Kiingereza limeendelea kuwapasua vichwa wanafunzi wa darasa la nne.

Hali hiyo imejidhihirisha tena kwa wanafunzi waliofanya mtihani wa upimaji wa taifa wa darasa la nne Novemba 23 na 24, mwaka jana baada ya kufaulu somo hilo kwa kiwango cha chini.

Akitangaza matokeo ya mtihani huo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mtihani la Tanzania (Necta), Dk. Charles Msonde, alisema somo lililoongoza kwa ufaulu ni Stadi za Kazi, Haiba na Michezo ambalo ufaulu wake ni asilimia 94.67 huku Kiingereza ikiwa ni asilimia 72.51.

Katika mtihani huo, wanafunzi 279,253 sawa na asilimia 27.49 walipata daraja E kwenye somo la Kiingereza, huku 261,025 sawa na asilimia 25.70 walipata daraja hilo kwenye mtihani wa Hisabati.

Alisema mtihani huo ulilenga kutoa tathmini endelevu ya mwanafunzi inayoweza kubaini umahiri wa juu wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), ambayo inawezesha kubaini maarifa, ujuzi na mwelekeo waliopata wanafunzi katika madarasa ya mwanzo.

Dk. Msonde alisema wanafunzi 1,054,191 walisajiliwa wakiwamo wasichana 542,071 sawa na asilimia 51.42 na wavulana 512,120 sawa na asilimia 48.58.
Alisema kati ya wanafunzi hao, 1,017,776 sawa na asilimia 96.55, walifanya upimaji, kati yao walikuwa 526,612 sawa na asilimia 97.15 sawa na asilimia 97.15 na wavulana walikuwa 491.164 sawa na asilimia 95.91.

Alisema wanafunzi 36,415 sawa na asilimia 3.45, hawakufanya upimaji, kati yao wasichana ni 15,459 sawa na asilimia 2.85 na wavulana 20,956 sawa na asilimia 4.09.

UFAULU

Katibu Mtendaji alibainisha kuwa wanafunzi 950,167 sawa na asilimia 93.36 waliofanya mtihani, walifaulu na kupata alama zenye daraja la kwanza hadi la nne, huku wanafunzi 67,547 sawa na asilimia 6.64, wakipata alama za daraja E lenye ufaulu usioridhisha.

Kwa mujibu wa Necta, mikoa 10 bora iliyofanya vizuri na idadi ya wanafunzi waliofaulu kwenye mabano ni Kagera (48,334); Kilimanjaro (34,361); Geita (44,118) na Njombe (18,416).

Mingine ni Iringa (25,177); Dar es Salaam (76,239); Arusha (37,571); Tanga (49,326); Mwanza (69,036) na Katavi (10,201).

Halmashauri 10 bora na idadi ya waliofaulu kwenye mabano ni Manispaa ya Bukoba (2,927); Makambako Mjini (2,648); Tanga Mjini (4,691); Chato (9,691) na Mafinga Mjini (1,942).

Nyingine ni Mufundi (6,419); Manispaa ya Ilala (14,271); Biharamulo (5,146); Hai (4,483) na Muleba (12,457).

Alizitaja shule 10 bora kitaifa na mikoa zilizopo kuwa ni St. Leo The Great na Acacia Land (Tabora); Kadama na Waja Springs (Geita); Twibhoki (Mara); Imani (Kilimanjaro); Msasa (Geita); St. Peter Claver (Kagera); Chalinze Modern Islamic (Pwani) na Modio Islamic (Kilimanjaro).

Wanafunzi 10 bora kitaifa na shule wanazotoka kwenye mabano ni Loi Kitundu (Fountain Joy), James Charles (St. Achileus Kiwanuka EMP), Erica Massaba (Tusiime), Kazungu Kazungu, Lightness Mpogolo, Michelle Meck, Mary Dickson na Luisa Aloyce (Waja Springs), Helieth Waryoba na Grace Manga (Twibhoki).

Wasichana 10 bora kitaifa ni Kitundu, Massaba, Mpogolo, Meck, Dickson, Aloyce, Waryoba, Manga, Angel Joseph (Twibhoki) na Francisca Kutageda (St. Leo the Great).

Kwa wavulana ni Charles, Kazungu, Joseph Kisinza (Msasa), James Mhele (Twibhoki), Bahati Msogela (Msasa), Steven Sige (Twibhoki), Ramadhani Issa (St. Leo The Great), Augustino Augustino, Jeremiah Magembe (Acacia Land English Medium) na John Joseph (Twibhoki).

Aidha, Baraza liliwataka walimu kuweka mkazo kufuatilia kwa karibu wanafunzi waliopata ufaulu wa chini ili wawasaidie kuimarika zaidi na kupata ufaulu wa juu zaidi.

Habari Kubwa