Kijana alivyopambana na mamba kwa saa 2 ziwani

28Feb 2021
Gurian Adolf
NKASI
Nipashe Jumapili
Kijana alivyopambana na mamba kwa saa 2 ziwani

MKAZI wa Kijiji cha Kabwe wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Thomas Kasagama (23), amenusurika kifo baada ya kupambana na mamba kwa saa mbili ndani ya maji.

Tukio hilo lilitokea Februari 25 majira ya saa 11 jioni baada ya kijana huyo kufika pembeni ya Ziwa Tanganyika na kuanza kuoga bila kuchukua tahadhari dhidi ya wanyama wakali.

Akizungumza kwa tabu katika Kituo cha Afya Nkomolo mjini Namanyere anakoendelea kupata matibabu, kijana huyo alisema kuwa muda mfupi baada ya kuanza kuoga, ghafla aliibuka mamba kwenye maji na kumvamia, aliangukia ndani ya ziwa.

Alisema baada ya kugundua kilichomvamia ni mamba, aliamua kuogelea na kuelekea sehemu yenye kina kirefu cha maji, akiamkini mamba hana uwezo mkubwa wa kumdhuru mtu aliye katika kina kirefu cha maji.

Kasagama alisema kuwa alipokuwa kwenye maji ya kina kirefu, mamba huyo alimfuata na akabahatika kumkamata miguu ya mbele na kumpindua juu chini na kumshika kwa nguvu huku akipiga kelele kuomba msaada.

"Nilipiga yowe na watu walifika, lakini kwa kuwa walikuwa hawana silaha yoyote, wakashindwa kuingia ndani ya maji wakihofia maisha yao.

"Walianza kupiga kelele huenda mamba angeogopa, lakini tuliendelea kuvutana naye mpaka alipochoka ndipo akaniachia.

"Baada ya mamba huyo kuondoka, ndipo nilipata msaada wa watu waliokuwa wakipiga kelele nikiwa tayari nimejeruhiwa sana kwenye mguu na mbavu za kushoto.

"Walinipeleka hospitalini, na baadaye gari la wagonjwa lilinisafirisha mpaka makao makuu ya wilaya, ninaendelea na matibabu hapa," alisimulia.

Mganga wa zamu wa Kituo cha Afya Nkomolo, Adelina Kizila, alisema mgonjwa huyo anaendelea vizuri na kwamba afya yake imeimarika tofauti na alipofikishwa katika kituo hicho.

Diwani wa Kabwe, Asante Lubisha, alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizo, aliwasiliana na Idara ya Afya wilayani kuhakikisha gari la kubebea wagonjwa linapatikana na kufika kwa wakati ili kuokoa maisha ya kijana huyo.

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda, akizungumzia tukio hilo, aliwaonya wakazi wa vijiji vya mwambao wa Ziwa Tanganyika kwenda kuoga ziwani kwa kuwa ni hatari kwa maisha yao.

Alisema wenye tabia ya kwenda kuoga ziwani, wanahatarisha maisha yao kwa kuwa sasa kuna ongezeko kubwa la wanyama wakali hasa mamba na viboko kwenye ziwa hilo.

Habari Kubwa