Kijiji kusahau vifo vya mama na mtoto

24Jun 2019
Zanura Mollel
LONGIDO
Nipashe
Kijiji kusahau vifo vya mama na mtoto
  • Ni baada ya mfadhili kujenga kituo cha afya katika kijiji cha Elerai

WANAWAKE wa kata ya Olmolog tarafa ya Enduiment waliokua wakisafiri Km zaidi ya 50 kufuata huduma za afya ya uzazi na wakati mwingine kusababisha vifo vya mama na mtoto wamemshukuru Diana Raleigh-

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Josephat Kandege na Diana Raleigh wakikata utepe KUZINDUA Zahanati ya olmot.

-raia wa Marekani kwa kujenga Zahanati na shule katika Kitongoji cha Olmoti kijiji cha Elerai kwa gharama zaidi ya Sh Bilioni 3.

"Tulikua tunatembea km 20 kufuata huduma za afya Ngarenairob iliyopo wilayani Siha, muda mwingine tulikua tunaenda hospitali ya mama Maria iliyopo kijiji cha Lerangwa zaidi ya km 18, huduma ya upasuaji tulikua tunafuata Kibong'oto au hospitali ya Magadini ambayo ipo km 50" Amesema mkazi wa kijiji Elerai, Nosimu Laizer

Akielezea mafanikio ya ujenzi huo wa Zahanati, Bi. Diana Raleigh amesema alikuja nchini mwaka 2009 kwa ajili ya mapumziko katika hifadhi ya wanayamapori Enduiment (EWMA) na kufanikiwa kutembelea maboma ya kimaasai na ndipo alipokutana na Mkunga wa jadi Bi.Yaya Ngulia

"Nilikutana na mkunga (Yaya Ngulia) akiwa na binti aliyekuwa anaumwa uchungu na ameshindwa kumzalisha hivyo akawa anaomba msaada wa usafiri ili aokoe maisha ya binti huyo, nilikubali kumsaidia lakini baada ya msaada huo nilimuuliza angependa nimsaidie nini zaidi alinambia anaomba niwajengee kliniki kwani wanatembea umbali mrefu sana kufuata huduma za afya," Amesema Raleigh na kuongeza kuwa;

"Yaya aliniambia yeye ni mkunga wa jadi na sasa nimezeeka sitaweza tena naomba utujengee kliniki kuokoa maisha ya wakina mama wajawazito na watoto hapo ndipo mwanzo wa ujenzi wa zahanati hii ulipoanza" Amesema 

Mama na mtoto wakiwa katika eneo la zahanati hiyo wakati wa ufunguzi.

Amedai kuwa ndani ya miezi sita kliniki ya mama na mtoto ilikamilika na baadaye waliongeza majengo mengine ikiwemo chumba cha upasuaji, wodi ya mama, baba na watoto na chumba cha kujifungulia wakina mama na kuweka vifaa vyote muhimu katika zahanati hiyo.

Raleigh amesema kuwa amehamasisha jamii juu ya afya na maambukizi ya Ukimwi na kuwataka kujitokeza kupima na kubaini hali zao pamoja na kuhakikisha wenye matatizo ya fistula na ugonjwa wa macho (trakoma) wanapata matibabu kwa haraka katika hospital ya KCMC iliypo Mkoa Wa Kilimanjaro.

"Kati ya watu  500 waliopima maambukizi ya Ukimwi walibainika watu sita pekee wakiwa na maambukizi, nimesaidia watu 1000 matibabu ya ugonjwa wa macho" Amesema Raleigh

Amedai kuwa wanawake wa jamii ya kifugaji walimwambia kuwa hawapo tayari kuwapeleka watoto wao shule kwani shule ipo mbali na makazi yao na kudai kuwa watabaki wakichunga Mifugo." Walivyonambia hivyo nilishirikiana na marafiki zangu kutoka Marekani tumejenga  Shule ya Msingi Olmot majengo sita kuna shule ya chekechea kuna vyoo vya kutosha na sasa watoto wanasoma " Amesema Raleigh

Raleigh ,hakuishia hapo alieleza vijana wa jamii ya kimaasai (Moran) zaidi ya 100 walimfuata na kumuomba kuwasomesha elimu ya watu wazima na kwenye shule hii pia wanafundishwa vijana hao (MEMKWA).

Habari Kubwa