Kijiji cha Dondo kupata zahanati baada ya miongo minne

23Sep 2021
Christina Mwakangale
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kijiji cha Dondo kupata zahanati baada ya miongo minne

KIJIJI cha Dondo, Kata ya Dondo, Tarafa ya Kisiju, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, kimepata matumaini mapya ya kuwa na zahanati baada ya kukosa huduma ya afya kwa miaka zaidi ya 40.

Mohamed Mtambo, akikabidhi fedha kwa kamati ya ujenzi kwa ajili ya kuchangia kujenga zahanati katika Kijiji cha Dondo, Mkuranga mkoani Pwani.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Dondo, Kata ya Dondo wilayani humo, Omary Seif Matope, amesema kata hiyo haijawahi kuwa na zahanati tangu Tanzania ipate uhuru wake mwaka 1961.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akipokea sehemu ya mchango kwa niaba ya kamati ya ujenzi wa zahanati hiyo,  Matope, amemshukuru mhandisi Mohamed Mtambo, aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Mkuranga, ACT Wazalendo ambaye amechangia shilingi 500,000 za ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Dondo.

"Hadi sasa wananchi kwa nguvu zetu tumeweza kufyatua tofari 2,800 huku mahitaji yakiwa ni tofari 10,500 hadi kukamilisha boma lote, kwa niaba ya wananchi wa Dondo namshukuru huyu kijana wetu kwa kutushika mkono ni rai yangu niombe wengine waige mfano huu wa kujitoa kwa ajili ya wengine.

"Kama mwenyewe alivyosema, maendeleo hayana chama, kwanza huu si muda wa kampeni, hatuna uchaguzi wowote hapa bali Dondo, kijana wetu ameguswa na hili kama Mtanzania yeyote na si vinginevyo," amesema Matope.

Mtambo amesema ametoa fedha hizo baada ya kuombwa na wananchi wa Kijiji cha Dondo, Kata ya Dondo Tarafa ya Kisiju Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, wiki iliyopita akiwa kwenye ziara ya kushukuru wananchi kwa kumpigia kura katika uchaguzi mkuu mwaka jana.

Amesema suala la kuchangia, kuhamasisha maendeleo lisihusishwe na itikadi zozote za kisiasa kwa sababu matatizo ya wananchi hususan suala la matibabu halichagui nani ataugua na wakati gani.

"Nimekuja hapa kuwashukuru kwa kunipigia kura mwaka jana, nimeona si haki kuwakimbia kwa kuwa hatukushinda, nialikeni kwa shughuli zozote za kijamii zikiwemo hitima, harusi, hata kuchimba mitaro ya ujenzi wa zahanati yetu nitakuja.

"Uzalendo kama lilivyo jina la chama chetu ni  pamoja na kurudi kutoa shukrani, kuishi na watu kidugu, kuwaunganisha na si kuwagawa" amesema Mtambo.

Awali akitoa kero na vikwazo vya ukosefu wa huduma za afya kijijini hapo,  mkazi wa eneo hilo, Maganga Lugutu amesema licha ya wananchi kujua umuhimu wa kuwa na zahanati, hali ngumu ya uchumi waliyonayo inawakwamisha kufikia lengo hilo.

"Changamoto kubwa tuliyo nayo kwa sasa ni kukosa huduma ya matibabu, mtu akiugua ni kazi kubwa kuweza kufika hospitali, kwa mfano umbali wa kutoka hapa Dondo hadi hospitali ya Wilaya ya Mkuranga kwa usafiri wa pikipiki ni Sh. 10,000 kwenda tu, bado dawa, vipimo.

“Mgonjwa akilazwa shida inakuwa kubwa zaidi tunaomba serikali ituangalie kwa jicho la pekee kutuongezea nguvu kwani tunateseka sana kwa kukosa zahanati" amesema Lugutu.

Amesema licha ya Kata hiyo kuwa na idadi kubwa ya watu, shule moja ya msingi na sekondari wamekuwa wakifuata matibabu kwenye kata zingine ambazo zipo umbali mrefu na kijiji chao.