Kikokotoo mafao bado kaa la moto

22Jun 2022
Salome Kitomari
Dodoma
Nipashe
Kikokotoo mafao bado kaa la moto

MBUNGE wa Viti Maalum, Ester Bulaya, amesema ni muhimu serikali ikaweka kikokotoo cha asilimia 50 badala ya asilimia 33 ya sasa ambayo kwa mtazamo wake inampunja mtumishi.

Vilevile, amesema fomula inayopaswa kutumika ni moja ya 480 kwa miaka 12.5 na siyo moja ya 540 kwa miaka 15.5.

Akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2022/23, Bulaya alisema fomula hiyo haiwezi kumsaidia mtumishi kwa kuwa anapata mkupuo mdogo, ambao humwezesha kujenga nyumba, kufungua biashara na kusomesha watoto wake.

Mbunge huyo alisema hali iko hivyo kwa kuwa serikali haionyeshi nia ya kulipa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii, huku akihoji ahadi ya Wizara ya Fedha na Mipango kutenga fedha kwa ajili ya kulipa madeni kwenye bajeti inayopendekezwa kwa mwaka 2022/23.

“Wakati Naibu Waziri wa Fedha na Mipango anajibu swali la Mbunge Halima Mdee kwenye majibu ya msingi, alisema Sh. trilioni mbili zitakuwapo kwenye bajeti hii kulipa deni la mifuko ya hifadhi ya jamii, mbali ya kwamba inalipwa kupitia hati fungani za muda mrefu lakini hii mifuko inahitaji fedha zao zilipwe, lakini hakuna hizo fedha,” alisema.

“Kwa sababu hamlipi madeni kwa wakati ndiyo maana mmeleta sheria ya kikokotoo cha kuwaminya watumishi. Siyo sawa, tuliambiwa tusubiri mnakutana na wadau, mmekutana nao na mmeleta asilimia 33 wakati cha mwanzo kabla ya 25 nyie ndiyo mliokibadilisha kutoka asilimia 50.

"Kwanini mnataka muwape asilimia 33 halafu mbaki na fedha yao nyingi? Watumishi ambao wana mishahara midogo, watumishi ambao kama hakuna Rais mwenye huruma wanaweza kukaa miaka mitano bila kuongezwa mishahara, mtumishi ambaye hajajenga, hajaanzisha biashara unamlipa asilimia 33 halafu unasema nyingine utamlipa taratibu na huko kwenye kumlipa umempunguzia miaka ya kumlipa baada ya kustaafu.”

Alitolea mfano mtumishi wa daraja la TGTS F1 anayepata mshahara wa Sh. 1,235,000 kwa kikokotoo cha asilimia 33 kiinua mgongo chake ni Sh. mil 47, huku akihoji kwa mshahara huo mtumishi wa mshahara mdogo atajenga nyumba saa ngapi na kuanzisha biashara.

Alisema kwa kikokotoo cha moja ya 540 kilichokuwapo mwanzo kwa mshahara huo angestaafu kwa kuchukua asilimia 50 angelipwa Sh. milioni 95 na angebaki na pensheni ya Sh. 500,000 kwa mwezi na angelipwa kwa miaka 15.

“Mnamtengenezea mazingira magumu na bado mnamkadiria afe haraka, hii siyo sawa. Na hawa wafanyakazi ndiyo wanatekeleza hii mipango tunayopitisha hapa,” alisema Bulaya.

Wakati mbunge huyo akiendelea kuchangia, Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, alimpa taarifa kuwa umri wa miaka 12.5 mtumishi atakayeishi zaidi ya miaka hiyo hata 30 ataendelea kulipwa.

Mbunge huyo alikataa kuipokea taarifa hiyo na kuhoji kwanini serikali imeweka miaka 12.5 badala ya 15, akisisitiza kuwa ni kwa sababu serikali imeikopa sana mifuko hiyo na hakuna fedha za kuwalipa wastaafu.

Kwa mujibu wa Bulaya, wadau walitaka fomula ya kikokotoo itumike mishahara minono na serikali ikasema itatumia mishahara bora 10 ndani ya miaka mitatu.

“Watumishi hawa wanaweza kukaa miaka mitano hawajaongezwa mishahara, siyo sawa, wanashindwa kusema kwa sababu mliwabana wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi kwenye vikao.

"Ndiyo maana vyama vya wafanyakazi haviwezi kutoka kusema, ninajua hii kanuni siyo msahafu, nendeni mkapitie wapeni asilimia 50 kama hawajajenga wajenge, waanzishe biashara na kusomesha watoto wao,” alisema.

Mbunge huyo alisema mifuko itaweza kulipa wastaafu vizuri, ikiwa serikali italipa madeni yake inavyotakiwa.

“Hamuwezi kuwalipa wastaafu wengi kwa sababu mifuko iko hohehahe, mtaweza kulipa ikiwa mtalipa madeni ya mifuko ikawa na uwezo,” alishauri.

Baada ya kusema hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, alisimama na kumpa mbunge huyo taarifa kuwa katika mchakato wa kufikia uamuzi ya kikokotoo, siyo kweli kwamba serikali ilivibana vyama vya wafanyakazi visizungumze.

“Wakati wa Mei Mosi, risala ya vyama vya wafanyakazi iliiomba serikali ifanye nini na waliweka wazi mchakato na walikubali ulikuwa shirikishi, namwomba Mbunge Bulaya aende kwenye risala ya vyama vya wafanyakazi kuna kila kitu,” alisema.

Hata hivyo, Bulaya alikataa taarifa hiyo na kusema suala la haki ya watumishi lisifanyiwe mchezo na kutaka wapewe asilimia 50, na kwamba ingekuwa haki wangepewa moja ya 480 na siyo moja ya 540.

Mjadala wa kikokotoo uliibuliwa na Nipashe mwaka 2017 baada ya kuchapisha ripoti iliyoonyesha jinsi fomula itakavyokuwa kutokana na kanuni za sheria mpya ya hifadhi ya jamii wakati huo.

Kutokana na jambo hilo kuibua mjadala mkali kitaifa, aliyekuwa Rais wakati huo, Hayati Dk. John Magufuli, alitangaza kuahirishwa kutumika kwa kikokotoo kipya hadi mwaka 2023.

Hivi karibuni, serikali ilitoa taarifa kuwa wamekubaliana kanuni mpya ya ukokotoaji wa mafao ya wastaafu iwe asilimia 33 badala ya 25 iliyopendekezwa awali.