Kikokotoo mafao chazidi kupingwa

07Dec 2018
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Kikokotoo mafao chazidi kupingwa

SIKU moja baada ya Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), kuomba kukaa meza ya mazungumzo na serikali kuhusu kikokotoo cha mafao ya pensheni, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimeibuka na kutaka kufanyiwa kazi haraka.

CWT imesema suala hilo linaleta ukakasi na kuumiza watumishi, hivyo linahitaji kufanyiwa kazi haraka na serikali.

Licha ya kutoa rai hiyo, CWT imewataka walimu kuwa watulivu kwa kuwa suala hilo linashughulikiwa na viongozi wa juu wa Tucta ambao wameomba kukutana na serikali, ili kujadili upya na kwamba wanaamini mwafaka utapatikana.

Pia imesema inaamini kwamba serikali kama ina nia nzuri na watumishi wake, hivyo  haiwezi kukwepa kukaa na Tucta ili kujadili na kufikia mwafaka ambao utakuwa na faida na maslahi ya pande zote mbili,  hatua ambayo itaondoa malalamiko kutoka kwa wafanyakazi.

Akizungumza katika kikao cha wenyeviti wa mikoa na makatibu wake, Rais wa CWT,  Leah Ulaya, alisema licha ya kuunga mkono tamko la Tucta, serikali inapaswa kulichukulia suala hilo kwa umuhimu wa kipekee, ili kupunguza kuleta malalamiko kwa wafanyakazi.

Alisema suala la kikokotoo ambalo kwa sasa limekuwa likichukua nafasi kubwa kuzungumziwa na watumishi wa umma na wafanyakazi wa sekta binafsi, limewaweka katika wakati mgumu viongozi wa vyama vya wafanyakazi na serikali, hivyo ni lazima lipatiwe ufumbuzi wa kina kutoka pande husika.

“Ni jambo ambalo ni gumu kwa sasa kwa sisi viongozi tunaongoza wafanyakazi na serikali haiwezi kulikwepa hili, lazima ikae meza moja na viongozi wa wafanyakazi kwa kuwa linahusisha watumishi wa umma na wasio wa umma, hivyo lazima kupatikana ufumbuzi wa kina,” alisema.

Sakala la mafao limekuwa gumzo katika ngazi mbalimbali baada ya kuanza kutumika sheria mpya kutokana na kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii na kubaki miwili. Mifuko hiyo mipya ni wa watumishi wa umma (PSSSF) na ule wa sekta binafsi (NSSF).

Tangu kutangazwa kwa kikokotoo kipya cha mafao ambacho kinaonyesha mfanyakazi kupata asilimia 25 ya malipo ya mkupuo, wadau mbalimbali wamekuwa wakilalamikia, huku ikidaiwa kuwa kanuni iliyotungwa ni kandamizi.

Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya, aliibua suala hilo huku akisema wabunge walifichwa juu ya suala hilo na hivi karibuni aliibuka tena na kusema anakusudia kuwasilisha hoja binafsi bungeni ili suala hilo lijadiliwe upya.     

Vyama vya wafanyakazi na makundi mbalimbali ya watu, wakiwamo wasomi, nao wamekuwa wakipinga hali inayoonyesha kuwa kanuni hiyo ya mafao inamuumiza mfanyakazi.  

MATATIZO YA WAFANYAKAZI

Kuhusu walimu, Rais huyo alisema walimu wanakabiliwa na matatizo mbalimbali yakiwamo maslahi, upandishwaji wa madaraja na ucheleweshwaji wa madai mbalimbali ambayo chanzo chake kikubwa wakiwa maofisa utumishi.

Alisema suala la maslahi ya walimu halikuanza kwenye uongozi wa awamu hii, bali viongozi wote waliopita walikuwa wakipambana na maslahi ya walimu na kwamba kunahitajika hekima na busara kwa ajili ya kutatua matatizo yote yanayowakabili walimu hapa nchini.

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Tixon Nzunda, alisema tayari serikali imeshaanza kurekebisha baadhi ya madai ya walimu ikiwamo marekebisho ya mishahara ya walimu 7,802 ambao walipandishiwa madaraja na kwamba kazi hiyo inaendelea na inatarajia kukamilika Januari, mwakani.

Nzunda aliwaonya maofisa elimu ambao wanaendelea kuwanyanyasa walimu kuacha mara moja tabia hiyo na kwamba yeyote atakayebainika kuendelea kufanya hivyo, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake ikiwamo kushushwa cheo.

Habari Kubwa