Kikosi kazi maoni ya siasa chabadili ratiba

09May 2022
Jenifer Gilla
Dar es Salaam
Nipashe
Kikosi kazi maoni ya siasa chabadili ratiba

KIKOSI Kazi cha kukusanya maoni ya wadau wa vyama vya siasa na demokrasia  kimebadili ratiba yake iliyotolewa tarehe 5 Mei, 2022.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Kikosi Kazi hicho, Sisty Nyahoza, wajumbe wa Kikosi Kazi wataanza kukutana na taasisi pamoja na watu binafsi badala ya vyama vya siasa kama ilivyoelezwa awali.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Kikosi Kazi kitaendelea kukutana na wadau mbalimbali wa demokrasia ya vyama vingi nchini kuanzia 10 Mei, 2022 kwenye ukumbi wa Chifu Adam Sapi Mkwawa, ofisi ndogo za Bunge jijini Dar Salaam.

"Siku hiyo Kikosi Kazi kitaanza kwa kukutana na Taasisi ya The Right Way kuanzia saa nne hadi saa tano asubuhi. Mchana kuanzia saa sita kitakutana na Msajili wa Vyama vya Siasa Mstaafu John Tendwa na kukamilisha ratiba yake kwa kukutana na Kituo cha Utawala Bora na Maendeleo (CEGODETA) kuanzia saa nane hadi tisa mchana,” alisema Sisty.

Vile vile taarifa huyo ilisema  kuwa siku ya Jumatano itakuwa zamu ya Jumuiya ya Wahindu Tanzania kuanzia saa nne hadi tano asubuhi. Mchana Kikosi Kazi kuanzia saa sita mchana kitapata wasaa kupokea maoni ya Sheikh Ponda Issa Ponda na baadaye Askofu Emaus Mwamakula wa Kanisa la Moravian.

Pia Alhamisi Kikosi Kazi saa nne asubuhi kitakuna na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe Benson Bagonza, mchana kuanzia saa sita itakuwa zamu ya Dk. Hellen Kijo Bisimba kuwasilisha maoni yake na baadaye kitapokea maoni ya mwanazuoni wa fani ya sheria Prof. Issa Shivji.

Taarifa iliendelea kueleza kuwa siku ya Ijumaa Kikosi Kazi kitapokea maoni ya mwanasheria na mwanahabari mkongwe Jenerali Twaha Ulimwengu na mwanasheria Fatma Karume kuanzia saa tatu hadi tano asubuhi.

Pia taarifa hiyo  inaonyesha wiki inayoanza Mei 16, Kikosi Kazi kitaendelea kukutana na taasisi mbalimbali na watu binafsi. Kikosi Kazi kitakutana na taasisi kama Chama cha Wakulima Tanzania (TASO), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mtandao wa Wanawake wa Katiba, Uchaguzi na Uongozi Tanzania.

Ilifafanua kuwa watu binafsi ni pamoja na mwanahabari Maria Sarungi, Wadhibiti na Wakaguzi Wakuu wa Hesabu za Serikali wastaafu Profesa Mussa Assad na Ludovick Utouh.
 

Habari Kubwa