Kikwete aona dalili usawa wa kijinsia

17Oct 2021
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kikwete aona dalili usawa wa kijinsia

MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais mstaafu, wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amesema usawa wa kijinsia unapiga hatua katika ngazi ya elimu ya juu nchini.

Alisema takwimu zinaonyesha kuna mafanikio katika kuelekea usawa wa 50 kwa 50, akibainisha kuwa kati ya wanafunzi 4,121 waliohitimu elimu ya juu chuoni huko mwaka huu wa masomo, wanaume ni 2,201 na wanawake ni 1,920, sawa na asilimia 46.6.

Kikwete alibainisha hayo jana mkoani Dar es Salaam katika Mahafali ya 51 ya chuo hicho na kusema kuwa idadi ya wanawake wanaohitimu vyuo vikuu inaendelea kuongezeka.

“Takwimu hizi zisipoelezwa hatuwezi kujua kama tunapiga hatua kubwa sana kwenye usawa wa kijinsia hadi ngazi ya elimu ya juu ambako wanafunzi wengi wa kike walikuwa hawafiki au kumaliza,” alisema Kikwete.

Alisema ngazi ya elimu ya msingi wanachukua wanafunzi 50 kwa 50 kwa sababu wanaandikishwa kwa usawa wa kijinsia.

“Wanapoanza kidato cha kwanza waanza wote sawa, kadri muda unavyokwenda wanapungua, sijui wanaenda wapi, huku ngazi ya chuo wanakuwa wachache. Lakini sasa tunaelekea hatua ya 50 kwa 50 kwenye suala la jinsia katika elimu ya juu," alisema Kikwete.

Makamu Mkuu wa UDSM, Prof. William Anangisye, alisema katika mahafali hayo, katika duru ya pili na ya tatu itakayofanyika Oktoba 20 mwaka huu wanafunzi 4,298 watahitimu na kutunukiwa shahada, stashahada na astashahada mbalimbali.

Alisema wahitimu hao ni kutoka katika Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia, Ndaki ya Insia, Ndaki ya Teknolojia za Habari na Mawasiliano, Shule Kuu ya Biashara, Shule Kuu ya Madini na Jiosayasi na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili.

Alisema wahitimu wengine ni kutoka Ndaki ya Sayansi za Kilimo na Teknolojia ya Chakula; Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi; Ndaki ya Sayansi za Jamii;  Shule Kuu ya Uchumi; Shule Kuu ya Sayansi Akua na Teknolojia ya Uvuvi; Shule Kuu ya Sheria; Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) na Taasisi ya Taaluma za Maendeleo (IDS) watatunukiwa tuzo zao katika duru ya tatu itakayofanyika Oktoba 20.

Aliwataka wanafunzi hao kuwa watu wa kutafuta fursa badala ya kusubiri fursa ziwafuate, jambo ambalo si rahisi kutokea ulimwengu wa sasa.

“Hata pale mtakaposhindwa kufikia mafanikio mliyotarajia, msife moyo, bali endeleeni kuwa na ari ya kujaribu tena na tena hadi mafanikio yapatikane,” alisema Prof. Anangisye.

Habari Kubwa