Kikwete atarajiwa kufungua mkutano wa kimataifa wa elimu bora

16May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kikwete atarajiwa kufungua mkutano wa kimataifa wa elimu bora

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, anatarajiwa kufungua mkutano wa kimataifa wa elimu bora ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) ambao utashirikisha wadau mbalimbali wa elimu kutoka serikalini, asasi na taasisi za kimataifa za ndani na nje ya nchi.

Mratibu wa Taifa TEN/MET, Ochola Wayoga.

Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Taifa TEN/MET, Ochola Wayoga, amesema mkutano huo wa kimataifa juu ya elimu bora unatarajiwa kufunguliwa na Rais mstaafu Awamu ya Nne, Kikwete siku ya Jumanne ya Mei 18 hadi Mei 20, 2021 katika ukumbi wa Kisenga jengo la LAPF.

Wayoga amesema Mkutano huo wa ubora wa elimu utajadili uwajibikaji wa pamoja katika kugharamia elimu bora nchini, ambapo utatoa fursa kwa wadau wa elimu ikiwepo serikali, wanachama wa mtandao, Washirika wa Maendeleo (Development Partners) pamoja na wadau mbalimbali wa elimu nchini kujadili hali ya ubora wa elimu kwa nia ya kuboresha zaidi.

Aidha, amewataja baadhi ya washiriki wa Mkutano huo ni pamoja na wajumbe kutoka Wizara ya Elimu, SayansinaTekinolojia, TAMISEMI, Mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau wa maendeleo, waheshimiwa Wabunge, Taasisi za elimu ya juu, tasisi za utafiti, Vyuo na shule za ufundi, Walimu, Wazazi na Wanafunzi.

“Mkutano huu utahudhuriwa pia na mabalozi wanao ziwakilisha nchi zao, wageni wengine mbalimbali kutoka nchi za ng’ambo, makampuni na taasisi za watu binafsi. Wajumbe takriban 200 wamethibitisha kushiriki katika mkutano huu; baadhi watakuwa wakishiriki kwa njia ya Mtandao,” amesema Wayoga

Habari Kubwa