Kilichojificha hasara ATCL

01Aug 2021
Sanula Athanas
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kilichojificha hasara ATCL
  • Mkurugenzi ataja shida nne
  • Rais Samia akiri, atasaidia

​​​​​​​MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Ladislaus Matindi, ameweka mezani mambo manne yaliyolifunga miguu shirika hilo kupaa kuelekea kwenye uwanja wa faida.

Sambamba na kadhia hizo, serikali nayo imetangaza rasmi kupokea wito wa 'kulifungua miguu' ulioko katika mpango kazi wa shirika hilo ambao uko mbioni kufanyiwa mapitio ya kina kabla ya kuidhinishwa rasmi.

Hayo ni miongoni mwa mambo makuu yanayohusu undani wa kinachoendelea ATCL yaliyowekwa hadharani juzi jioni jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya mapokezi ya ndege mpya ya tisa iliyonunuliwa na serikali kwa ajili ya kutumiwa na shirika hilo.

Katika hafla hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan alipokea ndege hiyo aina ya Bombardier DASH 8-Q400 iliyotoka Canada, akikiri kufahamu kwa kina yanayotokea ndani ya ATCL na kuweka bayana kinachoendelea kuhusu kulifungulia njia shirika hilo.

KIINI HASARA ATCL

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Matindi, alisema hasara ambayo imekuwa ikiliandama shirika hilo imetokana na madeni yaliyorithiwa.

Alisema madeni hayo yamekuwa na athari kwa shirika kushindwa kuongeza mtandao wa safari na kuongeza hasara kwenye uendeshaji kutokana na riba ambayo nayo imekuwa ikichukuliwa kama gharama za uendeshaji.

“Tunashukuru serikali kwa kuchukua hatua kulipa baadhi ya madeni hayo yakiwamo madeni makubwa," Matindi alisifu.

Aliitaja sababu ya pili kuwa ni muundo wa umiliki wa ndege ambao unazifanya kuwa mali ya serikali, hivyo kuhusishwa na madeni ya serikali.

“Athari ya muundo huo ni kushindwa kutekeleza utanuzi wa mtandao wa ATCL, kutotanua mtandao kunaongeza hasara katika uendeshaji kwani matumizi ya ndege yanaendelea kuwa ya chini,” alisema.

Mkurugenzi huyo alitaja sababu ya tatu kuwa ni muundo wa umiliki wa ndege kupitia mikataba ya ukodishaji kati ya ATCL na Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) ambao unaongeza gharama za uendeshaji na kuongeza hasara kwa shirika.

Matindi alisema mlipuko wa ugonjwa wa corona pia ni sehemu ya mzizi wa hasara, akifafanua kuwa ugonjwa huo umesababisha kupungua kwa idadi ya abiria wakati gharama za lazima za uendeshaji zikiendelea kuwapo.

“Hali hii imesababisha kuongezeka kwa hasara kama ilivyo kwa mashirika yote ya ndege duniani.

"Katika kipindi cha awali cha ufufuaji wa ATCL, serikali ilijikita katika kuanzisha shirika la kutoa huduma ya kulinunulia ndege, vilevile ilihakikisha kuna mifumo ya uendeshaji ya kuwezesha ndege hizo kufanya kazi.

"Jambo la muhimu katika uimarishaji wa ATCL ili iwe endelevu na shindani, ni kuhakikisha kampuni inaendelea kutoa huduma kwa tija kupitia ndege zinazohitajika kimkakati zaidi kibiashara na kiutalii kuiwezesha kuwa na miundombinu itakayopunguza gharama za uendeshaji ikiwamo karakana bora ili ndege zote zitengenezwe Tanzania," alisema.

Mkurugenzi huyo aliomba serikali kuirejeshea ATCL asilimia 20 za umiliki wa kampuni inayotoa huduma ya chakula kwenye ndege za serikali, akisisitiza uamuzi huo utawasaidia kupunguza gharama za uendeshaji.

Alisema ATCL imeongeza safari za kimataifa kutoka kituo kimoja cha Comoro hadi saba ambavyo ni Burundi, China, India, Uganda, Zambia, Zimbabwe na hivi karibuni inatarajia kuanzisha safari katika miji ya Kinshasa, Lubumbashi, Kalemie, Ndola, Nairobi, Dubai, Muscat na London.

RAIS SAMIA

Kwenye hotuba yake, Rais Samia alisema usafiri wa anga ni kichocheo muhimu cha maendeleo duniani kwa sababu usafiri huo ni wa haraka, salama na unotumiwa na watu wengi.

Alisema kuwa mbali na usafiri wa anga kusafirisha watu, pia ni muhimu katika kusafirisha bidhaa mbalimbali, hususan zinazoharibika haraka kama vile matunda, mboga za majani, samaki, maua na nyama.

Mkuu wa Nchi alisema serikali imeamua kununua ndege ya kusafirisha mizigo kwa sababu Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa matunda, mboga za majani na maua.

Alibainisha kwamba mwaka 2019, Tanzania iliuza nje ya nchi mazao yenye thamani ya takriban Dola za Marekani milioni 700 na inatarajia kuingiza Dola za Marekani bilioni mbili kufikia mwaka 2025, yaani katika miaka minne ijayo.

Rais Samia alisema ili nchi iweze kuvutia watalii wengi na kunufaika nao ni lazima iimarishe usafiri wa anga na ndiyo sababu ya uamuzi wa serikali kuifufua ATCL ikiwa na malengo ya kupokea watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025 kutoka watalii milioni 1.5 mwaka 2019.

Alisema serikali imeamua kuimarisha huduma za usafiri nchini ili inufaike na fursa za kijiografia za kupakana na nchi nane, ambazo kati yake, sita hazina bahari.

Rais Samia alizihimiza Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Uwekezaji na Sekta Binafsi kuweka mikakati ya kunufaika na fursa hizo ikiwamo kuanzisha kongani za kiuchumi kwenye maeneo kwa kuwa miundombinu ya usafiri inajengwa.

MPANGO KAZI

Rais Samia aliweka bayana kwamba katika miaka mitano ijayo, wanategemea kuliimarisha shirika hilo pamoja na sekta ya usafiri wa anga kwa ujumla.

Kuhusu vikwazo vinavyolikabili shirika hilo, Rais alisema serikali imepokea hoja zilizowasilishwa na Mkurugenzi Matindi na kuweka wazi Alhamisi alipokea mpango kazi wa shirika hilo.

Rais Samia alisema ofisi yake itaupitia na baadaye itakuwa na mjadala wa pamoja na ATCL na wizara husika kuona namna watakavyokwenda.

Pia alisema wanalifanyia kazi suala la hisa za ATCL kwenye kampuni inayotoa huduma ya chakula kwenye ndege hizo.

HASARA ILIYORIPOTIWA

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mku wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2019/20 iliyowasilishwa bungeni Aprili mwaka huu, inabainisha serikali ilitumia jumla ya Sh. trilioni 1.028 kununua ndege nane kati ya tisa zilizonunuliwa awali.

Vilevile, katika ripoti hiyo, CAG Charles Kichere, anabainisha kuwa ndani ya miaka mitano kati ya 2015/16 na 2019/20, ATCL ilipatiwa ruzuku ya Sh. bilioni 153.711.

CAG anasema ndani ya kipindi hicho, ATCL ilipata hasara ya Sh. bilioni 153.542, huku ndani ya mwaka mmoja wa fedha (2019/20), ikipata hasara ya Sh. bilioni 60.246.

Kwa mujibu wa CAG Kichere, hadi kufikia mwaka huo wa ukaguzi (2019/20), ATCL ilikuwa na mtaji hasi wa Sh. bilioni 472.853.

Habari Kubwa