Kilio tozo miamala ya simu chatulizwa

20Jul 2021
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Kilio tozo miamala ya simu chatulizwa

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema serikali imesikia kilio na maoni ya wananchi kuhusu tozo mpya ya miamala ya simu.

Amewaomba wananchi wawe watulivu wakati jambo hilo linatafutiwa ufumbuzi.

Aidha, alisema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameitisha kikao cha kujadili suala hilo ili kuona panapofaa kurekebisha.

Mwigulu alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku 19 tangu kuanza kwa utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2021/2022 baada ya Bunge kupitisha Sheria ya Fedha iliyofanya marekebisho na kuruhusu kodi na tozo mbalimbali 22.

Kodi ya miamala ilianza rasmi Julai 15, mwaka huu na kusababisha kuibuka mjadala mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, ujumbe mfupi na sauti mbalimbali za kueleza maumivu ya kodi hizo.

Kilio kikubwa kiko kwenye viwango vinavyotozwa huku mwananchi akikatwa fedha ya kampuni ya simu, kodi ya serikali na kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kiasi cha baadhi kuona bora kusafiri kupeleka fedha kwa muhusika kwa kuwa nauli ni ndogo zaidi.

Aidha, serikali ilitoa ufafanuzi wa kodi hiyo huku baadhi ya mawaziri wakiwaomba wananchi kukubali kufunga mkanda kwa ajili ya kujenga uchumi kwa kuwa fedha hizo zitaelekezwa kwenye barabara vijijini, shule na huduma za afya ambazo zinagusa wananchi wengi.

Mwigulu aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari akiambatana na Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Dk. Faustine Ndugulile.

“Kwa maaneo ambayo wananchi wametoa ushauri na kuelezea namna ambavyo jambo hili linawagusa, lakini pia tumepokea maeneo ambayo yanatakiwa kutoa elimu zaidi ili kujenga uelewa wa pamoja ikiwa ni pamoja na viwango vinavyokatwa kwa anayetuma na anayetoa, lakini kuhusu mantiki ya jambo lenyewe,” alisema Mwigulu.

Alisema jambo la tozo za miamala linatekelezwa kupitia sheria iliyopitishwa na Bunge, lakini kuna kanuni za utekelezaji zinazomhusu yeye kama Waziri wa Fedha na Mipango na maeneo mengine yanahusu Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, ambazo zitajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.

Alisema leo kutakuwa na kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kujadili suala hilo na pia kutakuwa na kikao kingine cha mawaziri wa wizara zote kuchambua kwa kina suala hilo.

“Lakini Mheshimiwa Rais naye alishaguswa na jambo hili, amesikia maoni ya Watanzania wote na yeye ametolea maelekezo kwamba tuyafanyie kazi maoni hayo,” alisema na kuendelea.

“Nitoe rai kwa wananchi kuwa watulivu kwenye jambo hili tutaendelea kuelezea na kutoa ufafanuzi kwenye kila maeneo yanayohitaji ufafanuzi na tutachukua hatua kwenye maeneo ambayo yanahitaji kuchukuliwa hatua ili ujenzi wa taifa letu uweze kuendelea kama ambavyo wananchi wamekuwa na shauku kubwa kuona ujenzi wa Taifa letu unaendelea kwa ajili ya maendeleo ya nchi.”

Hata hivyo, Dk. Mwigulu aliwaonya ambao wana nia mbaya ambao mara zote wanapenda kupotosha ama kubadili dhana ya maana halisi ya jambo ambavyo lilikuwa limekusudiwa na kuwataka wasifanye hivyo, kwani mambo haya yana maslahi mapana kwa nchi.

“Haya ni mambo ambayo ni ya kisheria, sheria za nchi zinatakiwa kuheshimiwa, ni mambo ambayo ni ya kikanuni na mambo yanayohitaji uelimishaji… tutaendelea kufafanua, lakini yale yanayotakiwa kufanyiwa kazi niwaahidi Watanzania tutaendelea kuyafanyiakazi kama ambavyo viongozi wetu wakuu wamesema,” alisisitiza.

Alisema tayari aliwapa maelekezo wataalamu wa mifumo kuangalia vipengele vya Sheria ya Mifumo ya malipo Serikalini pamoja na Sheria ya Mawasiliano ya Mtandao (EPOCA) inayoelezea kuhusu masuala ya miamala kwa njia ya mtandao na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kufikia muafaka wa jambo hilo.

Waziri Dk. Ndugulile alibainisha kuwa wizara yake pia ambayo inaguswa moja kwa moja na tozo hizo, imeendelea kupokea maoni na kuchakata taarifa mbalimbali tangu tozo hiyo ianzishwe na kumwahidi Waziri wa Fedha na Mipango kwamba atampa ushirikiano kuhakikisha kwamba maelekezo yaliyotolewa na viongozi yanatekelezwa.

Alirejea kutoa wito kwa Watanzania kuwa watulivu wakati jambo hilo linafanyiwa kazi na kusema kuwa serikali ni sikivu na itafikia muafaka mzuri.