Kilio uhaba wa mafuta kila kona

04Aug 2020
Na Waandishi Wetu
Katavi
Nipashe
Kilio uhaba wa mafuta kila kona

UHABA wa mafuta ya petroli na dizeli, umeyakumba maeneo mbalimbali nchini na kusababisha watumiaji wa vyombo vya usafiri kuzunguka vituo mbalimbali na kuambulia patupu, huku baadhi ya maeneo wakikaa kwenye foleni ndefu.

Madereva wa vyombo vya moto wakiwa katika foleni kubwa ya kununua mafuta ya petroli mjini Mpanda, mkoani Katavi jana, kutokana na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo. PICHA: NEEMA HUSSEIN

Pamoja na uhaba huo, bei ya mafuta imepanda kimya kimya tofauti na bei elekezi iliyotangazwa mwanzoni mwa mwezi uliopita hadi kufikia Sh. 1,837 kwa lita ya petroli, huku Mamlaka ya Udhibiti ya Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ikifafanua kuwa bei ilipanda kupisha uhaba na kulazimika kuruhusu shehena iliyokuwapo iliyoingizwa kwa bei ya juu kuuzwa kwa bei ya soko.

Aidha, katika eneo la Tabata baadhi ya vituo havijauza huduma hiyo kwa takribani wiki moja sasa, hali inayowasumbua watumiaji na kushindwa la kufanya. Hatua hiyo imesababisha baadhi ya madereva kuegesha vyombo vyao vya moto kwa muda wakisubiri hali hiyo kutengemaa.

Katika eneo la Tabata vituo vingi havikuwa na bidhaa hiyo kiasi cha kuwalazimu kuhama kutoka kituo kimoja kwenda kingine na bado hawakufanikiwa, huku waathirika wakuu wakiwa ni waendesha bodaboda na bajaji.

“Nimetembea kwenye vituo vitatu hadi sasa. Sheli (vituo vya mafuta vya Camel na Lake Oil Sanene na Oilcom Segerea hakuna mafuta. Wafanyakazi wapo lakini wanasema hakuna mafuta, kama unavyoona pikipiki yangu ina mafuta kidogo, kuliko niyamalize kwa kutafuta mafuta bora haya machache yahifadhi nipakie wateja,” alisema Shaibu Hussein.

Naye mmiliki wa gari dogo aliyekutwa kwenye kituo cha mafuta eneo la Tabata, Jane Mushi alisema alianza kutafuta huduma hiyo juzi jioni, lakini kila alikokwenda haikuwapo na wafanyakazi wa vituo hivyo walidai kuwa hawajapata mafuta kutoka kwa wasambazaji wakubwa.

Katika eneo la Kigamboni, madereva walionekana wakihaha kwa takribani siku tatu kutafuta bidhaa hiyo kiasi cha wengine kuegesha vyombo vya usafiri na wengine wakiomba kupunguziwa mafuta kutoka kwenye magari mengine ili kufikisha vyombo vyao nyumbani.

KATAVI

Mjini Mpanda, jana hali ilikuwa ngumu kiasi cha kutokea vurugu zilizovilazimu vyombo vya ulinzi na usalama kuingilia kati na kuwalazimisha wananchi kukaa kwenye mistari ili kupata huduma hiyo.

Nipashe ilishuhudia wananchi wakiwa kwenye misururu mirefu hasa wenye pikipiki na bajaji na wengi wakiamua kuegesha vyombo hivyo kutokana na kukosa huduma hiyo.

Kwa takribani siku tatu vituo vingi katika mji huo havina mafuta ya petroli isipokuwa kimoja ambacho kilifurika wanaohitaji huduma hiyo.

ARUSHA

Mkoani Arusha, tangu juzi hakuna huduma hiyo ndani ya jiji hilo, huku vituo vya barabarani kutoka Arusha mjini hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

“Tangu juzi hakuna mafuta kwenye vituo vya mafuta, mara kadhaa nimekwenda huduma wanasema hakuna mafuta, mfano jana nilikuwa naelekea KIA katika vituo vyote vya barabarani hakukua na mafuta,” alisema.

KAHAMA

Wilayani Kahama mkoani Shinyanga, huduma za usafiri ziliathiriwa kutokana na kukosekana kwa mafuta kwa takribani wiki moja hali iliyowalazimu baadhi kuviegesha.

Amos Ben, dereva wa pikipiki katika kituo cha mabasi mjini Kahama, alisema alikwenda kwenye vituo vingi lakini vimefungwa kwa kuwa hakuna mafuta hali iliyowafanya kutafuta kwa muda mrefu.

EWURA YANENA

Alipoulizwa na Nipashe kwa ujumbe mfupi wa maandishi, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti ya Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Titus Kaguo, alithibitisha uhaba huo, lakini akasema jambo hilo linakuzwa.

“Ni kweli kuna uhaba lakini watu wana-exagrate (wanakuza),” alisema.

Akizungumza na Nipashe kwa simu, Kaguo alifafanua wakati wa corona matumizi ya mafuta yalishuka kwa asilimia 17, lakini baada ya shughuli kurejea yalipanda huku kukiwa hakuna shehena mpya.

“Tuliagiza mafuta mengine, lakini meli ilikwama baharini kutokana na upepo wa monsoon, badala ya kufika Julai 27, imefika juzi. Hakuna mgomo wa wafanyabiashara ila shehena iliyokuwapo ilikwisha kutokana na mahitaji makubwa,” alifafanua Kaguo.

Aidha, alisema mahitaji ya mafuta yaliongezeka kutoka lita milioni 2.5 kwa siku hadi milioni 4.5 baada ya shughuli kurejea na kwamba uhaba uko kwenye petroli kutokana na kuwa na watumiaji wengi.

Kuhusu bei kupanda hivi karibuni, alisema baada ya kuona kuna uhaba na ndani ya siku tatu hakutakuwa na petroli, EWURA iliridhia shehena iliyokuwapo iliyoagizwa kwa bei ya juu kipindi cha nyuma kuuzwa kwa bei ya soko wakati huona ndiyo sababu ya bei kupanda kwa muda mfupi.

Kaguo aliwatoa hofu Watanzania kuwa hakuna uhaba mkubwa kiasi hicho kwa kuwa kuna meli tatu zimefika na kwamba watu wanakuza huku akitoea mfano eneo la Kigamboni lenye vituo 14 na vitatu pekee havina Petrol na kwamba kusema hakuna mafuta ni kupotosha.

Juni 29, mwaka huu, EWURA ilisema maghala ya mafuta yana lita 92,435,539 za petroli ambazo zingetosheleza kwa siku 25 na diseli walikuwa na lita 147,398,593 zilizotosheleza kwa siku 29.

Mamlaka hiyo ilisema ina shehena ya petroli yenye tani 39,772 iliyotegemewa kuwasili nchini Julai Mosi, mwaka huu.

Bei ya mafuta mafuta hayo iliporomoka kutoka zaidi ya Sh. 2,000 kwa lita ya petroli, kufikia Sh. 1,520 na disel 1,546 kwa Jiji la Dar es Saalam.

Pia Juni 30, mwaka huu, mamlaka hiyo ilitangaza tena bei mpya ambayo ilikuwa na ongezeko la kati ya Sh. 170 hadi 173 kwa petroli na disel, na kufikia Sh. 1,520 hadi 1,693 kwa Jiji la Dar es Salaam.

Kila Jumatano ya mwanzo wa mwezi, EWURA hutoa bei elekezi ya mafuta ya petrol, na dizeli na mafuta ya taa kulingana bandari inayohudumia eneo husika. Bandari hizo ni Mtwara, Tanga na Dar es Salaam.

Imeandikwa na Salome Kitomari (DAR), Shaban Njia (KAHAMA), Neema Hussein (KATAVI) na Allan Isack (ARUSHA)

Habari Kubwa