Kilio ukosefu maji chatawala bungeni

11May 2021
Salome Kitomari
DODOMA
Nipashe
Kilio ukosefu maji chatawala bungeni

UKOSEFU, upotevu wa maji na madeni ya makandarasi jana vilitawala mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji, wabunge wakitaka hatua zichukuliwe haraka kuongeza kasi ya upatikanaji wa maji nchini ili kuwaondolea kero wananchi.

Watunga sheria hao walitaka gharama za kuunganishiwa maji kukatwa kwenye ankra na wananchi kuruhusiwa kununua vifaa kuliko utaratibu wa sasa wa kulazimishwa kununua kwenye mamlaka za maji.

Pia walisema kiwango cha upatikanaji wa maji kinachotajwa na wataalamu kuwa ni zaidi ya asilimia 86 kwa mijini na asilimia 72.3 vijijini, hakiakisi kiasi hicho na inawezekana kuwa ni chini ya asilimia 50.

Mbunge wa Viti Maalum, Esther Bulaya (CHADEMA), alisema upotevu wa maji ni tatizo sugu tangu mwaka 2010 na kwamba kati ya mamlaka za maji 23, mamlaka 21 zina upotevu wa maji kupita kiasi.

Kwa mujibu wa Bulaya, mwaka 2018/19 serikali ilipata hasara ya Sh. bilioni 77 na mwaka 2019/20 Sh. bilioni 155 na kwamba kwa miaka miwili zilipotea Sh. bilioni 332 ambazo zingechimba visima au kugharamia miradi mingi kwenye majimbo na kumtua mama ndoo.

“Tunajua kuna upotevu baada ya kukokotoa yanayozalishwa, miundombinu ya maji ni chakavu, ni muhimu kuziba mianya ya maji kupotea.

“Kanuni ya usambazaji wa maji serikali inapaswa kupeleka ruzuku kwenye mamlaka za daraja A hadi C na mwaka huu serikali imeshindwa kupekela fedha kwenye mamlaka 10, tunashindwa kutengeneza, huku hatupeleki fedha na tunataka kumtua mama ndoo?" Alihoji.

Kuhusu madeni ya maji, mbunge huyo alisema kuna Sh. bilioni 148 ziko nje huku serikali ikidaiwa Sh. bilioni 64, na Sh. bilioni 83 ni madeni ya viwanda na wateja wa kawaida.

“Serikali kutolipa makandarasi kwa wakati na kufanya riba kuongezeka ni tatizo lingine kubwa sana, mfano mradi wa Ruvu Chini riba imefikia Sh. bilioni 3.9, zingelipwa kwa wakati zingekamilisha miradi mingine kweye maeneo ya Moshi, Arusha na Dar es Salaam," alisema.

Alisema taarifa za Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) zilionyesha upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo Mkoa wa Pwani ni asilimia 96, lakini Mdhibiti na Mkakuzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alivyopita alibaini nia asilimia 53 na huenda ikashuka zaidi na kuwa asilimia 50," alisema.

Aliitaka serikali kukamilisha mradi wa muda mrefu wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda kata 14 za Mji wa Bunda. Mbung wa Viti Maalum, Esther Matiko (CHADEMA), alisema Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa ulijiwekea malengo ya kufia mahitaji kwa asilimia 85 vijijini na 90 mjini, huku miradi 1,423 ilitekelezwa na visima zaidi ya 100,00 na kwamba nusu yake havitoi maji.

“Fedha zinazopelekwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji hazina uhalisia na zinapotea, zinapelekwa kidogo. Wabunge wanafurahi kuwa mwaka mpya kuna miradi mingi na fedha zimetengwa lakini tatizo ni utekelezaji.

"Kuna miradi 85 ilibidi irudiwe tena, mfano mradi wa Dodoma ulitumia Sh. bilioni 2.2 na zinahuishwa tena Sh. bilioni 2.2, hizi fedha zinakwenda wapi?" Alihoji.

Kuhusu mradi wa miji 28 wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 460, alisema kuna taarifa kuwa idadi itapunguzwa huku umbali na mtandao wa maji ukiwa ni uleule, akitaka uchunguzi kufanyika juu ya mabadiliko hayo.

“Tunaomba sana ufanyike uchunguzi tena kupitia Kamati ya Maji, waunde tume kupitia huu mradi, ili tuende na utaratibu wa mwanzo na siyo ya sasa kupunguza miji, na ikiwezekana ipate maji, mtandao wa maji umepungua sana kama ilikuwa kata nane, zitaingia kata mbili.

“Kuna ubadhirifu wa fedha, bila kung’oa mizizi bado upatikanaji wa maji utakuwa ni historia katika maeneo mengi, tunaomba uwajibikaji kwa ambao wamehusika kwa upotevu wa fedha za miradi ambayo inahuishwa tena na kutumia mamilioni ya fedha," alisisitiza.

Mbunge wa Chemba, Mohamen Moni (CCM), alisema wilayani kwake wanaopata maji hawafiki asilimia 42 na kwamba kuna miradi iliyoshindikana.

Mbunge wa Nkasi Kusini, Vicent Mbogo (CCM), alisema katika jimbo hilo kuna kata tatu hazijawahi kupata mradi wowote wa maji na kwamba gari lake limegeuka gari la wagonjwa kubeba wananchi waliojeruhiwa na mamba wakati wanakwenda kutafuta maji.

“Wabunge wanasema wana miundombinu chakavu, kwangu haipo kabisa, wanasema kuna wanaokunywa maji ya njano kwangu ni tope, kuna mabomba ya maji yaliletwa yamekaa kwa zaidi ya miaka minane. Waziri ninaomba upimwe kwa kuleta maji Nkasi," alisema.

Mbunge wa Makambako, Deo Sanga, alisema wakandarasi katika jimbo lake wanadai serikali jambo lililosababisha miradi mingi kukwama na kutaka hatua kuchukuliwa ili wananchi wapate maji.

Mbunge wa Mbozi, George Mwanisongole, aliitaka serikali kuruhusu wananchi kukatwa kwenye ankara za maji gharama vifaa kwa ajili ya kuunganishiwa maji kwa kuwa kiasi cha Sh. 500,000 ni kikubwa kwa mwananchi wa kawaida.

Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama, alitaka wananchi waachwe wanunue vifaa vya kuunganishiwa maji na mamlaka zikague kama vimefikia viwango ili kuondoa malalamiko na kuona kama kuna upigaji, wakinunua wao gharama zinakuwa kubwa na usumbufu, na mfumo wa ununuzi ni tatizo.

Habari Kubwa