Kilo 88.27 za Heroin, Methamphetamine zakutwa ndani ya gari

17Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kilo 88.27 za Heroin, Methamphetamine zakutwa ndani ya gari

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imefanikiwa kukamata kilo 88.27 za dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphetamine zikiwa ndani ya gari aina ya Toyota Prado iliyokuwa imetelekezwa barabarani.

Gerald Kusaya.

Taarifa hiyo imetolewa na Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo, Gerald Kusaya, amesema dawa hizo zimekamatwa Juni 2, mwaka huu majira ya saa 7 usiku katika eneo la Kimara Korogwe, huku akisema kuwa kukamatwa kwa dawa hizo kumetokana na ushirikiano wa mamlaka hiyo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya TRA kulitilia shaka gari hilo na kuanza kulifuatilia.

"Dereva wa gari hilo baada ya kugundua anafuatiliwa alitelekeza gari na kukimbia, baada ya upekuzi wa kisheria kufanyika ndani ya gari kulipatikana na mifuko mikubwa mitatu aina ya sandarusi (viroba) na ndani yake kukiwa na pakti 12 za dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa kilo 12.25 pamoja na kontena za plastiki 73 ndani yake kukiwa na dawa aina ya Methaphetamine zenye uzito wa kilo 76.02," amesema Kamishina Jenerali Kusaya.

Amesema upelelezi bado unaendelea ikiwemo kugundua mwenye gari hilo na mtandao wake na kwamba Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vipo macho, havijalala, pia amewaasa wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya waache kwani , hawatabaki salama.

"Ama zao, ama zetu lakini watambue Mamlaka tuko kazi muda wote na lengo letu ni kukomesha kabisa biashara hii haramu. Tunaomba Wananchi waendelee kutoa taariffa ili kwa pamoja tushirikiane kukomesha dawa hizo,"amesema Kusaya.

Habari Kubwa