Kimbunga Kenneth chaanza kuonekana Mtwara, Serikali yatoa tahadhari

25Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Kimbunga Kenneth chaanza kuonekana Mtwara, Serikali yatoa tahadhari

Serikali imeelekeza mamlaka zote na wananchi wote wa mikoa ya Mtwara, Lindi na mikoa iliyo jirani wanaoishi kando kando ya bahari ya Hindi kuchukua tahadhari na kuondoka mara moja katika maeneo hayo kutokana na tishio la  kimbunga Kenneth kinachotarajiwa kutokea katika maeneo hayo.

Kauli hiyo  imetolewa leo Aprili 25 bungeni na Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi Ajira na watu wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati akitoa kauli ya serikali juu ya tahadhari ya kutokea  kimbunga iliyotolewa na mamlaka ya hali ya hewa nchini kuanzia usiku wa tarehe 24 mpaka 26 ambapo serikali imeshauri shughuli za majini kama uvuvi na usafiri wa majini na anga zisitishwe katika maeneo hayo katika kipindi hicho kutokana na hali ya hewa mbaya inayotabiriwa na athari zinazoweza kutokea kwa wananchi.

Aidha amezitaka kamati za maafa na uongozi katika ngazi zote za serikali hasa mikoa ya Mtwara na Lindi kuendelea kutoa tahadhari kwa wananchi ili kupunguza athari za kimbunga hicho huku akitoa rai kwa  taasisi za serikali na binafsi kuendelea kufuatilia hali hii kwa kina na kujiandaa kutoa msaada wa kibnadamu mara utakapohitajika.

Amesema ofisi ya waziri mkuu idara ya maafa itaendelea kuchukua hatua stahiki katika kuendelea kuchukua tahadhari na kuhakikisha wananchi na mali wanakuwa salama licha ya majanga yanayotabiriwa.

Kimbuka Keneth kinatarajiwa kutokea Pwani ya Kusini ya Tanzania kwa kasi ya KM 130 kwa saa umbali wa Kilometa 75 ya mkoa wa Mtwara ikitarajiwa kuleta athari mbalimbali kama  mtawanyiko wa mafuriko,upepo mkali unaoweza kusababisha uharibifu wa makazi na mali.

 

 

Habari Kubwa