Kina Kitilya waachiwa kisha kukamatwa tena

12Jan 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Kina Kitilya waachiwa kisha kukamatwa tena

ALIYEKUWA kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya, na wenzake wawili waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka manane likiwamo la utakatishaji fedha, jana walifutiwa kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kisha kukamatwa na kusomewa upya mashtaka 58. 

Mbali na kukamatwa tena, washtakiwa hao walisomewa mashtaka na Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) huku wakiongezwa watuhumiwa wawili ambao ni Kamishna wa Sera na Uchambuzi wa Madeni kutoka Wizara Fedha na Mipango, Bedason Shallanda na msaidizi wake, Alfred Misana.
 
Kitillya na wenzake  ambao ni maofisa wa benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Solomon, walifutiwa kesi hiyo  baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP)  kuomba kuondoa shtaka hilo mahakamani na kwamba hana nia ya kuendelea nayo. 
 
Maombi hayo yaliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Hashimu Ngole, na Mahakama ikakubali na washtakiwa wakafutiwa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili. 
 
Washtakiwa hao walifutiwa mashtaka hayo chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) Sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
 
Uamuzi wa kufutiwa kesi hiyo ulifikiwa  jana  na Hakimu Mkazi, Salum Ally baada ya DPP kueleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
 
Wakili Ngole akisaidiwa na wenzake Pendo Mangole na Patrick Mwida, alidai mahakamani hapo kuwa DPP hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya washtakiwa hao.
 
"Taarifa hii ya kutokuendelea kwa shauri hili mbele ya mahakama yako, imeletwa chini kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) Sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002," alidai  Ngole.
 
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Ally alisema kutokana na maombi hayo, mahakama imeifuta kesi hiyo.
 
Washtakiwa hao baada ya kufutiwa kesi hiyo, walikamatwa tena na kupandishwa kizimbani kisha kusomewa mashtaka mapya 58 yakiwemo 49 ya utakatishaji fedha.
 
Washtakiwa hao na wengine wawili walioongezwa, walisomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali Mkuu, Ngole mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustina Mmbando. 
 
Katika mashtaka hayo washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kughushi, moja la kuongoza uhalifu,  49 utakatishaji fedha, mawili ya kutoa nyaraka za uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanyanyifu moja na shtaka la kutoa nyaraka kwa nia ya kumdanganya  Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango. 
 
Akiwasomea mashtaka hayo, Wakili Ngole alidai kuwa  kati ya Machi 15, 2013 na Januari 10, 2014 ndani ya jiji la Dar es Salaam, kwa nia ya kudanyanya, washtakiwa wote walijipatia Dola za Kimarekani milioni sita wakionesha kuwa zilikuwa malipo ya ada ya uwezeshaji wa upatikanaji wa mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya Egma (T) Ltd. 
 
Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wakili Ngole alidai kuwa washtakiwa wote, Machi 18, 2013 na Januari 10, 2014 wakiwa jijini Dar es Salaam walitakatisha Dola za Marekani 6,000,000 kwa kuzitoa fedha hizo kupitia njia ya benki kwa jina la Enterprises Growth Market Advisors (EGMA) katika benki ya Stanbic Tanzania.
 
Pia katika kosa la kusababisha hasara kwa serikali, Wakili Ngole alidai kwa pamoja washtakiwa hao,  Mei 1, 2012 na Juni 1, 2015 wakiwa jijini Dar es Salaam, walijipatia Dola za Marekani  6, 000,000 kama ada ya mkopo uliochukuliwa na Serikali ya Tanzania kutoka katika asilimia 1.4 hadi 2.4 na kusababisha serikali ipate hasara ya Dola za Marekani milioni sita.
 
Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza shauri hilo.
 
Wakili Ngole alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na Hakimu Mmbando aliharisha kesi hiyo  hadi Januari 24, 2019 itakapotajwa. 

Habari Kubwa