Kina Mbowe wakata rufani Mahakama Kuu

09Apr 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kina Mbowe wakata rufani Mahakama Kuu

VIGOGO wanane wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwamo Mwenyekiti Taifa, Freeman Mbowe, wamekata rufani Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kupinga hukumu ya kulipa faini ya jumla ya Sh.milioni 320 au kwenda jela miaka mitano kwa Kila kosa.

Vigogo hao wa Chadema walikutwa na hatia Machi 8, mwaka huu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, hivyo kutakiwa kwenda jela au kulipa jumla ya kiasi hicho cha fedha.

Rufani hiyo iliyosajiliwa kwa namba 76 mwaka huu, iliwasilishwa na wakili wa walalamikaji, Peter Kibatala, ikiwa na sababu 14, bado inasubiri kupangiwa jaji wa kuisikiliza.

Kwa mujibu wa hati ya rufani, walalamikaji wanadai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, ilikosea kuwatia hatiani Mbowe na wenzake kwa sababu haikuchambua ushahidi wa Jamhuri wakati wa kuandika hukumu hiyo.

Hoja nyingine, Mahakama ya Kisutu katika hukumu yake haikuonyesha sababu zilizopelekea washtakiwa kutiwa hatiani.

"Upande wa Jamhuri ni jukumu lao kuthibitisha makosa bila kuacha shaka na kwamba si kazi ya mshtakiwa kujitetea," inaeleza sehemu ya hoja za walalamikaji.

Hoja nyingine, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, hakutilia maanani utetezi wa washtakiwa akiwamo Esther Matiko na John Mnyika katika ushahidi wa Jamhuri hakuna ulipoeleza kama washtakiwa walikuwapo kwenye tukio.

Pia, mahakama ilikosea kuwatia hatiani washtakiwa katika shtaka lililokuwa na mashtaka manne ndani yake ikiwamo kufanya maandamano, kusababisha kifo cha Akwilina Akwilin, kusababisha askari polisi wawili kujeruhiwa.

Hoja nyingine kwamba mahakama ilipokea CD iliyoonyesha maandamano ya washtakiwa kinyume cha sheria na kwamba utaratibu wa kisheria haukufuata kielelezo hicho kilipokelewa kiholela.

Mbali na Mbowe, Matiko, Mnyika, washtakiwa wengine ni Mchungaji Peter Msigwa, Halima Mdee, John Heche,
Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya.

Pia alikuwapo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, ambaye hata hivyo, alishahamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika kesi ha msingi, Mbowe na viongozi wenzake walishtakiwa kwa mashtaka 12 ya uchochezi na moja la kula njama.

Mashtaka 12 yaliyokuwa yakiwakabili katika shtaka la kula njama, wanadaiwa kufanyika kati ya Februari Mosi na 16, mwaka 2018 wakiwa Kinondoni Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani kwa kutenda kosa la jinai na kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Bulaya anakabiliwa na shtaka la kushawishi kutenda kosa la jinai ambapo anadaiwa Februari 16, mwaka huo, katika viwanja vya Buibui Kinondoni Dar es Salaam, alishawishi wakazi wa Kinondoni kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Nchimbi alidai washtakiwa wote Februari 16, mwaka huo, wakiwa katika barabara ya Kawawa, Kinondoni Mkwajuni, Dar es Salaam, kwa pamoja wakiwa walikusanyika kutekeleza lengo kinyume cha sheria, kwa kuendelea na mkusanyiko hali iliyowafanya watu waliokuwa kwenye eneo hilo waogope uwezekano wa kuwapo uvunjifu wa amani.

Habari Kubwa