Kina Papa Msofe waunganishwa kesi ya uhujumu

12Feb 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kina Papa Msofe waunganishwa kesi ya uhujumu

WAFANYABIASHARA Marijani Msofe, maarufu Papa Msofe (53), na Fadhil Ibrahim (61), wameunganishwa na Wakili wa Kujitegemea, Abdul Lyana (37), katika kesi ya uhujumu uchumi.

Watatu hao wanakabiliwa na mashtaka ya kuratibu genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia fedha na kutakatisha zaidi ya Dola za Marekani, 26,250 (Sh. milioni 60.375).

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustina Mmbando wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Wakili wa Serikali, Gloria Mwenda, alidai upande wa Jamhuri unaomba kubadilisha hati ya mashtaka na kuwaunganisha washtakiwa wawili na mwenzao katika kesi hiyo.

Hakimu Mmbando alisema mahakama yake imekubali washtakiwa kusomewa hati mpya ya mashtaka.

Mwenda alidai kuwa kati ya Januari Mosi na Desemba 30, 2019, jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote watatu waliongoza genge la uhalifu kinyume cha sheria kwa lengo la kujipatia fedha.

Katika shtaka la pili na la tatu, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza, washtakiwa wote watatu, walitakatisha fedha baada ya kujipatia kwa njia ya udanganyifu zaidi ya Sh. milioni 60 kutoka kwa Yasser Abdelhamad kwa kijifanya kuwa wangemuuzia tani 25 za madini ya shaba huku wakijua si kweli.

Hata hivyo, washtakiwa hao hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Upande wa utetezi ulidai kuwa unaomba muda wa kuwasiliana na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kujadiliana kuhusu washtakiwa kukiri mashtaka yao.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa hauna pingamizi na ombi la utetezi.

Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa Februari 17 mwaka huu na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.

Habari Kubwa