Kinachojiri mpakani ni hujuma utalii -RC

21May 2020
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Kinachojiri mpakani ni hujuma utalii -RC

MKUU wa Mkoa wa Arusha, amesema ofisi yake imebaini mbinu chafu zinazofanywa kwa lengo la kuharibu biashara ya utalii nchini, hususani katika jiji hilo la kiutalii.

Mrisho Gambo amesema moja ya mbinu walizobaini ni madereva 19 wa malori kutoka Tanzania, ambao walipimwa Kenya na kuonekana wana maambukizo ya virusi vya corona, lakini walipopimwa nchini majibu yakaonyesha hawana maambukizo.

Taarifa iliyotolewa jana jijini hapa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Mkoa huyo, ilisema ofisi yake imejiridhisha kuwa hizo ni mbinu chafu za majirani kutaka kuua soko la utalii katika Mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla.

Katika taarifa yake hiyo, Gambo alisema waliamua kuchukua upya baadhi ya sampuli za madereva 19 raia wa Tanzania, waliopimwa katika Mpaka wa Namanga upande wa Kenya na kuzipeleka Maabara Kuu ya Taifa iliyoko jijini Dar es Salaam, ambako majibu yalionyesha kuwa madereva hao hawakuwa na maambukizo ya ugonjwa huo.

“Hizi ni mbinu chafu za nchi jirani za kutaka kuua soko la utalii katika Mkoa wetu wa Arusha na Tanzania kwa ujumla, kwa sababu baada ya vipimo vyao kudai kuwa madereva wetu 19 wana maambukizo ya ugonjwa wa Covid-19, tulijiridhisha.

"Tulichukua sampuli za madereva hao na kuzipeleka kwenye Maabara Kuu ya Taifa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupimwa na majibu yalitoka kuwa madereva hao walikuwa 'negative' (hawana maambukizo)," Gambo alisema katika taarifa yake hiyo.

Kwa mujibu wa Gambo, kutokana na ongezeko la maambukizo ya ugonjwa wa Covid-19 kupitia mipakani, Mkoa wa Arusha umeanzisha utaratibu wa kuchukua sampuli za madereva wa malori wanaopita Mpaka wa Namanga kutoka Kenya tangu Mei 14 mwaka huu.

Alibainisha kuwa sampuli zote zilizochukuliwa na wataalamu wa afya kuanzia siku hiyo hadi Mei 18 mwaka huu zimepelekwa Maabara Kuu ya Taifa jijini Dar es Salaam na kupata majibu ya vipimo husika.

“Utaratibu wa kuchukua sampuli ili kupima Covid-19 kwa madereva wa malori wanaotoka Kenya, ulianza kutumika rasmi Mei 14 mwaka huu na majibu yalikuwa kama ifuatavvyo:

"Madereva 44 kutoka Kenya waliochukuliwa sampuli Mei 14, mwaka huu na majibu yalitoka Mei 16, mwaka huu, madera 11 raia wa Kenya walikuwa na maambukizo ya covid-19, dereva mmoja kutoka Uganda na madereva wawili ambao majina ya nchi yao yanahifadhiwa na madereva 30 hawakuwa na maambukizo.

“Mei 16 mwaka huu, madereva 23 kutoka Kenya walichukuliwa sampuli ambazo pia zilipelekwa Maabara Kuu ya Taifa na majibu yalitoka Mei 19, mwaka huu, ambapo madereva 10 raia wa nchi hiyo walikutwa na maambukizo hayo na madereva 13 hawakuwa na maambukizo."

Gambo pia alisema Mei 18 mwaka huu, madereva 11 kutoka nchi jirani walichukuliwa vipimo na majibu yake yatatangazwa baada ya majibu kupatikana kutoka Maabara Kuu ya Taifa ya jijini Dar es Salaam.

“Tumechuka uamuzi huu ili kuwalinda wananchi wetu dhidi ya maambukizo ya ugonjwa wa Covid-19 kutoka Kenya pamoja na kuimarisha usalama wa afya ya wananchi wetu kama sehemu ya maandalizi ya kupokea watalii msimu msimu utakapoanza mapema mwezi Juni mwaka huu,” alisema.

Gambo alisisitiza kuwa kuanzia sasa, madereva wote watakaopimwa na kukutwa na maambukizo ya Covid-19, hawataruhusiwa kuingia nchini wala kwenda Kenya na kwamba Mkoa wa Arusha unaendelea kuchukua tahadhari na kudhibiti maambukizo ya ugonjwa huo kwenye Mpaka wa Namanga.

Kwa takriban wiki mbili sasa, kumekuwa na malalamiko ya madereva wa Tanzania kulazimishwa kupimwa mpakani Namanga na wataalamu wa afya kutoka Kenya na kudaiwa wengi wao wana maambukizo ya virusi vya corona.

Habari Kubwa